}

WAZIRI SIMBACHAWENE AKABIDHIWA VIFAA TIBA KWAAJILI YA POLISI NA MAGEREZA.

 Na. Geofrey Jacka - Dodoma.


Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Mh. George Simbachawene leo Septemba 15, 2021 amepokea vifaa Tiba kutoka katika shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwaajili ya vituo vya Afya vya Jeshi la Polisi na Magereza, kupitia mradi wa 'USAID POLICE AND PRISONS ACTIVITY'.


Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo Mh. Simbachawene amesema kuwa, vifaa hivyo vitakwenda kuboresha huduma za Afya ndani ya Majeshi hayo pamoja na jamii inayovizunguka vituo vilivyolengwa kupatiwa vifaa hivyo.


"Kwa niaba ya Majeshi haya Polisi na Magereza, natoa Shukrani Sana kwa THPS pamoja na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa uamuzi wa kutoa msaada wa vifaa hivi, ni msaada mkubwa utakaoenda kuboresha kwa kiasi kikubwa sekta ya Afya ndani ya Majeshi yetu haya, pamoja na jamii nzima kwaujumla, hivyo nitoe wito kwa vituo vitakavyo kabidhiwa vifaa hivi, wakavitunze ili viweze kudumu na kuendelea kutoa huduma" aliongeza Simbachawene.



Kwaupande wake Mkurugenzi wa THPS, Dr. Redempta Mbatia amesema kuwa, kupitia mradi wa 'USAID POLICE AND PRISONS ACTIVITY', THPS imekuwa na dhamana ya kufanya kazi na Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi ili kusaidia kuboresha huduma za UKIMWI na Kifua kikuu kwa Askari, familia zao na jamii inayozunguka vituo vya Afya 64.


Naye Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Bi. Kate Somvongsori amesema kuwa, Serikali ya Marekani kupitia Shirika hilo inayo furaha kuifadhiri THPS katika kutekeleza mradi huo, na kuwezesha ununuzi wa mashine 10 za kisasa Gene Expert na Hadubini 10 za i-LED ambazo zitagawiwa kwa vituo vya kutolea huduma 14 vilivyopo katika Mikoa 14.
Awali akimkaribisha Waziri Simbachawene, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee, amesema kuwa, msaada huo utalinufaisha Jeshi la Magereza, kwani limekuwa na dhamana pia ya kutoa huduma ya Afya kwa wateja wake ( Wafungwa), licha ya Maafisa, askari na familia zao, huku akiwakaribisha wadau hao kutumia maeneo ya Makao makuu ya Magereza, kwa shughuli zao mbalimbali pindi watakapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo.


Hafla hiyo ya Makabidhiano imefanyika Makao Makuu ya Jeshi la Magereza Msalato Jijini Dodoma, ambapo vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 400 vimekabidhiwa.







No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.