}

WAZIRI SIMBACHAWENE AIPA 'TANO' MAGEREZA.

Na. Stephan Ngolongolo -Dodoma
Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi George Simbachawene (mwenye suti ya bluu) akiweka jiwe la Msingi katika kituo cha Biashara cha Jeshi la Magereza, eneo la Isanga Jijini Dodoma.


Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mh.George Simbachawene (Mb), leo Agosti 17, 2021 ameweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa kituo cha biashara katika eneo la Isanga Jijini Dodoma, (Isanga Prison Business Centre).

Akizungumza katika hafla hiyo ya uwekaji jiwe la Msingi  Waziri Simbachawene amelipongeza Jeshi la Magereza kwa uwekezaji huo mkubwa, na amewataka watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Jiji la Dodoma kuja kuangalia fursa za uwekezaji katika eneo hilo.

“Nafahamu ipo miradi  mbalimbali ya uwekezaji katika maeneo ya  Jeshi la Magereza, niseme tu siku ya kwanza nilipotembelea  Gereza Mbigili nilisema kauli yangu  fikra mpya  mtazamo mpya kufanya kazi kwa bidii  na kujitegemea neno hilo lilikuja tu  nilivyoona hatua za awali tu mlivyonunua kijiko linafanya  kazi kubwa, nikajua hapa shughuli  imeanza”alisema Simbachawene. 

Kwa upande mwingine Simbachawene amesema, mabadiliko yoyote yanaweza kuletwa na ‘leadership’ (uongozi) hivyo lazima ujitoe, na hao viongozi wanaotaka mabadiliko  wakati fulani watalaumiwa sana, lakini kikubwa ni kuangalia matokeo yakoje.

“Ishini katika viapo  vyenu wewe umeajiriwa kama askari songa mbele, mwanajeshi akipewa amri na kiongozi wake anatekeleza,nyinyi askari watiifu, historia itatuandika kwamba tulifanya nini, kwaiyo Kama viongozi msiogope lawama" alisema Simbachawene.


Aidha Simbachawene amesema kuwa, ameridhishwa na uwekezaji unaofanywa na Magereza, tena kwa kiasi kidogo Cha fedha, huku akishindwa kuficha hisia zake na kusema kuwa eneo hilo la biashara la Magereza lina mvuto mkubwa na wa aina yake, ambalo linaweza kuwa bora zaidi Tanzania.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee amesema, wameshaagiza matrekta kumi na tano pamoja na Magari mengine yapo njiani, huku akieleza kuwa malengo ya Jeshi ni kuwa na miundombinu  rafiki ya kuitoa Magereza hapa ilipo,  na mwangaza umeshaonekana. 

“Ndugu zangu tunatengeneza miundombinu na tunafanikiwa, huo muda mnaosema miaka kumi naona mbali sana, mimi nasema miaka mitatu mje muone maajabu hapa" alisema CGP Mzee.


Aidha Mzee amezungumzia matumizi ya “video conference” magerezani amesema, Teknolojia ni nzuri hivyo jitihada zinaendelea ili kuifanya Teknolojia hiyo iweze kutumika katika Magereza yote nchini, huku suala la  ugonjwa wa corona akisema,  Jeshi linaendelea kufuata miongozo inayotolewa na wizara ya Afya, kwa kufuata taratibu zote.


Awali akisoma taarifa kwa mgeni rasmi mkuu wa Magereza mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi wa Magereza Keneth Mwambinje ambaye pia ni msimamizi mkuu wa mradi huo amesema, mradi huo  unahusisha fremu za maduka, chumba cha kuoneshea bidhaa mbalimbali za Magereza (showroom), sehemu ya kuoshea magari (car wash), kumbi za starehe na shughuli zingine mbalimbali zinazotarajia kufanyika katika kitiuo hicho, huku gharama za mradi huo zikiwa ni shilingi Milioni mia tano na hamsini na moja, laki nne na elfu sabini,baadhi ya sehemu zimeshaanza kutumika.


No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.