}

MAGEREZA YAIBURUZA NGOME, SMZ, MASHINDANO YA MAJESHI.

 Na. Geofrey Jacka - Dodoma.



Mashindano ya Majeshi yameendelea kutimua vumbi Jijini Dodoma, kwa kuzikutanisha timu za Majeshi zinazoshiriki katika Michezo mbalimbali.

Mashindano hayo yalianza rasmi Agosti 05, 2021, katika viwanja vya Shule ya Mtakatifu Gasper ambapo baadhi ya timu za Jeshi la Magereza zimeendelea kuonesha ubabe ikiwemo Netball, Kikapu, Volleyball, na Handball.


Katika Mchezo wa Kikapu wanaume, Magereza imeiburuza SMZ kwa vikapu 84, huku SMZ wakiambulia 62, na katika Mchezo wa Netball Magereza wanawake wameiburuza Ngome magoli 52 kwa 46.

Akitoa tathmini ya Michuano hiyo Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP. Bertha Minde, amesema kuwa Hali ya Mashindano ni nzuri licha ya changamoto ya kupoteza baadhi ya Michezo, hivyo amewataka wachezaji kutokata tamaa.

"Katika Michezo kuna vitu vitatu lazima ukubaliane navyo, Kuna kushinda, kutoka sare na kushindwa, kwaiyo niwatake wachezaji msikate tamaa, bado tuna nafasi ya ubingwa katika baadhi ya Michezo, na mkumbuke Michezo ni Afya", alisema SACP. Minde.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza SACP. Bertha Minde (wa tatu kutoka Kulia waliokaa) akifuatilia Michuano ya Majeshi Jijini Dodoma.

Michuano ya Majeshi imekuwa ikifanyika kila mwaka, ikiwa ni njia ya kuboresha mahusiano baina ya Majeshi hayo, huku ikiwaimarisha Askari kiafya na kiakili, na itaendelea kutimua vumbi kwa zaidi ya wiki moja.












No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.