}

"UNYANYAPAA MOJA YA CHANGAMOTO INAYOWAKUMBA WAFUNGWA WANAPORUDI URAIANI" - SACP. KAZIULAYA

 

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, SACP. Justine Kaziulaya, akishiriki mkutano wa wakuu mbalimbali wa idara ya Magereza wa Mataifa ya Shelisheli, Mauritius, Israel na Tanzania, kwa njia ya Mtandao.


Imeelezwa kuwa unyanyapaa ni moja ya changamoto kubwa kwa wafungwa wanaorudi uraiani.

Hayo yameelezwa leo na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza(SACP) Justine Kaziulaya katika mawasilisho yake katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao kati ya Tanzania, Israeli, Mauritius na Shelisheli.

Katika mawasilisho hayo Kamishna Kaziulaya alisema kuwa kutokana na unyanyapaa wafungwa wengi wanaomaliza vifungo vyao hawajisikii amani kurudi katika jamii zao, hivyo kulazimika kwenda kuishi mbali na nyumbani kwao hali inayopelekea kurudia kufanya makosa na kujikuta wakirudi tena magerezani.

Kamishna Kaziulaya alizitaja baadhi ya changamoto nyingine kuwa ni mtizamo finyu wa jamii kuhusu adhabu mbadala (Altenative punishments), ukosefu wa mitaji na vitendea kazi kwa wafungwa hao wanaorejea uraiani.

Akihitimisha mawasilisho yake, Kamishna Kaziulaya alisema kuwa suala la kuwapokea tena wafungwa wanaorejea uraiani ni suala linalohitaji mtazamo wa pamoja na hasa ikizingatiwa kuwa suala la urekebishaji wa tabia zao ni suala mtambuka ambalo linahitaji ushirikishwaji wa jamii nzima.

Aidha, katika mkutano huo ulioandaliwa na Idara ya Magereza ya Ushelisheli kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ushelisheli , washiriki walipata fursa ya kuwasilisha, kujadiliana na kubadilishana uzoefu wa kazi mbalimbali zinazofanywa na Idara ya Magereza, katika suala zima la urekebishaji wa wafungwa katika nchi zao.

 Mkutano  huo umefanyika katika  kumbukizi ya siku ya Mandela inayoadhimishwa kila mwaka kimataifa ikiwa mi katika kukumbuka mchango wake katika Magereza.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.