}

JESHI LA MAGEREZA LAJIDHATITI KUPAMBANA NA CORONA MAGEREZANI.

 Na. Geofrey Jacka - Dodoma

Msemaji wa Jeshi la Magereza SACP. J. Kaziulaya akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ugonjwa wa Corona Magerezani.

Msemaji wa Jeshi la Magereza Tanzania bara SACP. J. Kaziulaya, leo Julai 29, 2021 ametoa taarifa kuhusu hali ya Ugonjwa wa Corona (Covid 19) katika Magereza.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika ofisini kwake, makao makuu ya Jeshi la Magereza Msalato Jijini Dodoma, Kaziulaya amesema, Jeshi la Magereza limepokea na kufanyia kazi muongozo wa namba moja uliotolewa na Kamati ya  Kitaifa iliyoundwa na Mh. Rais Samia Suluhu, kutafuta namna sahihi ya kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kudhibiti mikusanyiko isiyo ya Lazima.

Pipa la maji kwaajili ya kunawa kabla ya kuingia Gerezani, katika Gereza Msalato Jijini Dodoma.

"Sisi Magereza tumepewa dhamana ya kuwapokea na kuwahifadhi Wafungwa na Mahabusu, kwahiyo lazima tuchukue tahadhari Sana, kwasababu kila siku tunapokea watu wapya, hivyo tunafuata miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara ya Afya, na tunaendelea kutoa elimu kwa maafisa na Askari pamoja na Wafungwa na Mahabusu namna ya kujikinga" aliongeza SACP. Kaziulaya.

Akizitaja hatua zinazoendelea kuchukuliwa mpaka Sasa ni pamoja na kuweka vifaa vya kupimia joto la mwili 'Thermoscanners' kwaajili ya kuwapima wote wanaingia katika maeneo ya Magereza, kupunguza idadi ya waageni (Visitors) wanaokuja kuwatembelea Wafungwa na Mahabusu hadi kufikia wawili kwa wiki, kupunguza muda wa mazungumzo kati ya mfungwa na ndugu aliyekuja kumtembelea hadi kufikia dakika tano, pamoja na kuendesha kesi kwa njia ya mtandao (video conference).


Aidha Kaziulaya amesema mpaka Sasa hakuna taarifa yoyote ya uwepo wa wagonjwa wa Corona Katika Magereza yote hapa nchini.

"Tunawajulisha kuwa Jeshi la Magereza litaendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga kama inavyoelekezwa, na kubwa zaidi ni kwamba mpaka Sasa hakuna taarifa yoyote ya uwepo wa Mgonjwa wa Corona Katika Magereza yetu hapa nchini" Aliongeza Kaziulaya.


No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.