}

WAZIRI SIMBACHAWENE AINGILIA KATI MGOGORO WA ARDHI JESHI LA MAGEREZA NA WANAKIJIJI.

 Na. Geofrey Jacka - Dodoma

Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi George Simbachawene (katikati), akizungumza na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee, walipotembelea Kijiji Cha Chihikwi, kushoto pichani ni Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavunde.


Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi George Simbachawene (Mb), amefanya ziara ya kikazi makao makuu ya Jeshi la Magereza Jumatano Juni 23, 2021 na kisha kwenda katika kijiji cha Chihikwi kwa lengo la kutatua mgogoro wa mipaka baina ya wakazi wa Kijiji hicho na Jeshi la Magereza.

Akizungumza na wanakiji mara baada ya kufika kijijini hapo Simbachawene alisema, lengo la Ziara yake ni kwaajili ya kutatua mgogoro ulipo na amefika hapo kwaajili ya kutoa hitimisho, ambapo aliwaeleza wanakijiji kuwa eneo hilo ni mali ya Jeshi la Magereza, hivyo  Jeshi hilo lipo tayari kutoa hekari ishirini na kisha kila mwanakijiji kupewa eneo lenye ukubwa wa Robo hekari, Jambo ambalo lilipingwa vikali na wanakijiji hao.
Waziri Simbachawene (wa kwanza kushoto) akimsikiliza Mwananchi wa Kijiji Cha Chihikwi, wakati wa mkutano baina yake na wanakijiji hao.

Baadhi ya wanakijiji waliopata nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo wamesema kuwa, eneo hilo ni mali yao tangu enzi na enzi, hivyo hawapo tayari kupewa Hekari 20 kama zawadi au kuonewa huruma, hivyo wao ndio wenye mamlaka ya kuwapa ardhi Magereza, kwakuwa ni mali yao.
Mara baada ya kusikiliza hoja za wanakijiji hao, Waziri Simbachawene alihitimisha mkutano huo kwa kuwataka wawe watulivu kwani ameyachukua maoni yao na anakwenda kuyafanyia kazi.

"Niseme kitu kimoja Sasa ndugu zangu, nimeyachukua maoni yenu, naenda kuyafanyia kazi, na nawaahidi kwamba nitakuja tena hapahapa chini ya mti huu ili kutoa muafaka wa Jambo hili, Ila niwaambie kuwa, ardhi ni mali ya Serikali kwa mujibu wa Sheria za nchi yetu, na hivyo Mwananchi atafidiwa kulingana na kile alichokiendeleza juu ya ardhi hiyo" Alisema Simbachawene.
Wananchi wa Kijiji Cha Chihikwi wakiwa katika mkutano na Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi George Simbachawene.

Mgogoro huu wa Ardhi umeibuka Mara baada ya Jeshi la Magereza kuanza kupitia mipaka ya maeneo yake, ambapo kaya 86 ndizo zilibainika kujimegea eneo la Jeshi na kuanzisha makazi ndani ya eneo hilo katika kijiji cha Chihikwi jijini Dodoma.
Waziri Simbachawene akizungumza na Mbunge wa Dodoma mjini Mh. Anthony Mavunde (wa kwanza kushoto) pamoja na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee (wa pili Kulia) Mara baada ya mkutano na wanakijiji wa Chihikwi kumalizika.

Askari wa Kikosi maalumu Cha Jeshi la Magereza akiimarisha ulinzi wakati wa mkutano wa Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi George Simbachawene na wanakijiji wa Chihikwi jijini Dodoma.






























No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.