}

BODI YA PAROLE YA TAIFA YAKUTANA MAKAO MAKUU YA MAGEREZA.

 Na. Geofrey Jacka - Dodoma

Bodi ya Parole inayoongozwa na Mwenyekiti wa bodi hiyo Mh. Augustino Lyatonga Mrema, ikiendelea na kazi ilipokutana Makao Makuu ya Magereza Jijini Dodoma.

Bodi ya Parole ya Taifa leo Juni 29, 2021, imekutana na kufanya kikao katika ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, ikiwa ni mpango wake wa kila mwaka katika utendaji wa Majukumu ya Bodi hiyo.

Akizungumza na wakati wa kikao hicho Mwenyekiti wa Bodi hiyo Taifa Mh. Augustino Lyatonga Mrema amesema, lengo la Bodi hiyo kukutana ni kuyapitia na kuyajadili Majalada ya Wafungwa waliopendekezwa kuachiwa kupitia huduma hiyo na kisha kuyatolea mapendekezo Majalada yaliyokidhi vigezo.

"Leo hapa tulikuwa na Majalada ya Wafungwa 76, nashukuru wajumbe wamefanya kazi nzuri na tumefanikiwa kupendekeza Wafungwa 70, na Wafungwa Sita pekee ndio hawajapendekezwa kwakutokidhi vigezo vinavyohitajika". Amesema Mrema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa Mh. Augustino Lyatonga Mrema (kushoto) akipitia nyaraka wakati wa kikao cha Bodi hiyo, Kulia ni Katibu wa Bodi ambaye pia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee.

Aidha Mrema amesema kuwa, Magereza yamekuwa na Msongamano mkubwa hasa wa Mahabusu, ambao hufikia Elfu kumi na Saba, hivyo amelitaka Jeshi la Polisi kukamilisha upelelezi kwa haraka ili Mahakama nayo iweze kutoa haki kwa haraka, kwani idadi hiyo ya Mahabusu ni kubwa kuizidi idadi ya Wafungwa, ukizingatia Mahabusu hawatumiki katika uzalishaji ndani ya Magereza.

"Mahabusu wamefikia Elfu kumi na Saba, ni idadi kubwa Sana hii, ukizingatia Mahabusu wanalelewa hawafanyi uzalishaji wowote, ningeziomba taasisi Kama Polisi na Mahakama kufanya kazi zao kwa haraka ili haki itolewe kwa wakati, itasaidia kupunguza Msongamano wa Mahabusu Magerezani". Aliongeza Mrema
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Parole wakimsikiliza kwa Makini Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mh. Mrema (hayupo pichani), wakati wa kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Magereza.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Meja Jenerali Suleiman Mzee, ambaye ni Katibu wa Bodi ya Parole amesema, kutokana na Msongamano wa Wafungwa na Mahabusu Magerezani, Jeshi la Magereza lipo kwenye mkakati wa kujenga Magereza mapya kila Wilaya, na kuongeza Magereza ya Ngome, ambapo tayari Magereza Manne yamesha jengewa Ngome. 

"Hiki ni kikao Cha 44 cha Bodi, nashukuru nimeenda vizuri, hii ni njia moja wapo ya kupunguza Msongamano Magerezani, Kama mnavyojua zipo njia nyingi ikiwemo ya Msamaha wa Rais, lakini sisi Kama Jeshi pia tuna mkakati kuhakikisha tunajenga Magereza kila Wilaya, lengo sio kuongeza watu bali ni kuwatawanya Wafungwa katika Magereza hayo, ili wasirundikane katika Gereza moja". Alisema CGP Mzee.
Wajumbe wa Bodi ya Parole wakiwa katika kikao cha Bodi hiyo.

Aidha CGP Mzee amesema kuwa, Bodi hiyo hukutana Mara nne kwa Mwaka, ila inaweza kupungua kutokana na Ukosefu wa Wafungwa wanaopendekezwa katika kujadiliwa, na kuhusu ugonjwa wa Corona kutokana na Msongamano Magerezani Mzee amesema kuwa, zinafuatwa kanuni zinazotolewa na Serikali katika kuhakikisha ugonjwa huo hauingii Magerezani.

"Hii Bodi inatakiwa kukaa Mara nne kwa Mwaka, lakini wakati mwingine hazitimii kutokana na ukosefu wa Wafungwa wanaokidhi vigezo vya kusamehewa kupitia huduma hii, lakini wakiwepo ndio Kama hivi tunakutana, na baada ya hapa, haya majina tuliyopendekeza yatawasilishwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kwaajili ya kuwaachilia rasmi". Aliongeza CGP Mzee.









No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.