KAMATI YA BUNGE 'YATINGA' MAGEREZA, ZUNGU APIGA SALUTI.
Na. Geofrey Jacka - Dodoma
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee, (wa pili Kulia) akimpigia Saluti Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, ulinzi na usalama, Mh. Mussa Hassan Zungu, Mara baada ya kamati hiyo kuwasili Ofisi za Makao makuu ya Jeshi la Magereza Msalato Dodoma.
Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, ulinzi na usalama, leo Juni 19, 2021 imefanya ziara ya kikazi katika makao makuu ya Jeshi la Magereza yaliyopo Msalato Jijini Dodoma, kwa lengo la ukaguzi wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa na Jeshi hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Mussa Hassan Zungu.
Akizungumza kuhusu Ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Mh. Zungu amesema, ni ziara ya kawaida ambayo Kamati yake imekuwa ikifanya kwa taasisi inazozisimamia, huku akiweka wazi juu ya kuridhishwa na Maendeleo yanayofanywa na Jeshi la Magereza, chini ya Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, Meja Jenerali Suleiman Mzee.
"Hii ni ziara ya kawaida ya kikazi, lakini niseme tu, kamati imekagua na kuridhishwa na Mambo yanayo fanywa na Magereza, tena naweza kusema Jenerali Mzee ni Kama amechelewa kuja ndani ya Jeshi hili, nampongeza sana, amefanya mambo makubwa". Alisema Zungu.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya nje, Ulinzi na Usalama, akichangia hoja katika kikao cha Kamati hiyo, pamoja na Maafisa wa Ngazi za juu wa Jeshi la Magereza.
Aidha Mh. Zungu amesema kuwa, kamati yake imezipokea changamoto zilizoelezwa na CGP mzee, ikiwemo upimaji wa maeneo ya Jeshi hilo, Ulipwaji fidia kwa maeneo yaliyoporwa, huku akilichukulia kwa uzito suala la Kiwanda Cha Sukari, katika eneo la Mbigiri mkoani Morogoro, na Kiwanda Cha Viatu Cha Karanga mkoani Kilimanjaro ambapo Magereza imekuwa na Asilimia chache za umiliki.
"Changamoto alizozisema Mzee tumezibeba, tutazifanyia kazi, lakini kwasasa naweza kusema Magereza ipo vizuri, kwakuwa Mambo mengi ambayo tuliyakosoa tulipotembelea mwanzoni yamerekebishwa" alisema Zungu.
Kwaupande wake CGP Mzee amesema kuwa, ni faraja kutembelewa na viongozi wa Ngazi za juu wa Serikali, huku akipokea kwa furaha Kauli ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, iliyoeleza kuridhishwa na Mwenendo wa Jeshi hilo.
"Ni faraja Sana kutembelewa na viongozi wa namna hii, na Kauli ya Mh. Zungu imeongeza chachu ya kuendelea kufanya kazi zaidi, kwa maana Askari wetu pamoja na Wafungwa, kule kujitoa kwao kumetambuliwa, hivyo niwatake waendelee kufanya kazi zaidi" Alisema CGP. Mzee.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee, akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani), Mara baada ya kumalizika kwa Ziara hiyo.
Aidha CGP. Mzee amesema kuwa, wakati alipoteuliwa kuliongoza Jeshi la Magereza, kazi kubwa ilikuwa ni kubadilisha fikra za Maafisa na Askari wa Jeshi hilo, ambapo amesema kuwa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kazi Sasa zinafanyika kwa ufanisi kila mkoa ambao Magereza ipo.
"Mwanzoni ilikuwa ni kubadilisha kwanza 'Mindset' (fikra) ili tusonge mbele, hilo limefanikiwa, ndio Mana Sasa kila mkoa kuna miradi inaendelea kuhakikisha Jeshi linajitegemea, ili kutoiingizia madeni Serikali, hivyo kwa kujitegemea kwetu tumeweza kuokoa fedha za Serikali zaidi ya Bilioni moja" alisema CGP. Mzee.
Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge wakiwa katika kikao Cha pamoja na Maafisa wa Ngazi za juu wa Jeshi la Magereza.
Wajumbe waliopata fursa ya kuchangia hoja katika kikao hicho walisema kuwa, wameridhishwa na Mwenendo wa Jeshi la Magereza kwa Sasa, huku wakisema kuwa Jeshi hilo bado lina kazi ya kufanya ili kusonga mbele zaidi, huku mmoja wa wajumbe akieleza hisia zake katika upande wa uboreshwaji wa Michezo, ambapo alisema Jeshi lifanye umuhimu wa kujenga Shule, na vituo vya kukuza vipaji, kwani Wana Michezo wengi wamekuwa wakitokea Majeshini.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo (wa pili kushoto) akitoa maoni wakati wa kikao na viongozi wa Ngazi za juu wa Jeshi la Magereza.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, wakifuatilia kwa makini maelezo yanayotolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee (Hayupo pichani) wakati wa kikao Cha Kamati hiyo na Viongozi wa Ngazi za juu wa Jeshi la Magereza.
Jeshi la Magereza limeendelea kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa ya Maendeleo katika maeneo yote nchini, ambapo jijini Dodoma pekee, inaendelea na Ujenzi wa Kiwanda kikubwa Cha kutengeneza Samani, Kiwanda cha kuoka Mikate, Ukumbi mkubwa wa Mikutano na Sherehe, ujenzi wa nyumba Bora za makazi ya maafisa na askari, Hostel kubwa kwaajili ya Timu ya mpira wa miguu ya Jeshi hilo, Tanzania Prison Fc, ambayo inatarajiwa kuhamishiwa jijini Dodoma Mara baada ya kukamilika kwa hostel hiyo, Karakana kubwa ya Jeshi, huku CGP. Mzee akieleza kuwa suala la ujenzi wa makazi ya Askari ni zoezi la nchi nzima.
No comments