JINSI CGP MZEE ALIVYO MUIBUA MKURUGENZI WA UFUNDI KATIKA MICHEZO WA JESHI LA MAGEREZA.
Na. Geofrey Jacka - Dodoma
Mkurugenzi wa Ufundi katika Michezo wa Jeshi la Magereza Wdr
Kelvin Fredinand Tresphory.
Jeshi la Magereza nchini Tanzania, limekuwa ni mdau mkubwa katika Michezo, likiwa na timu zinazo shiriki Ligi mbalimbali huku timu ya mpira wa miguu ya Jeshi hilo Tanzania Prisons Sc ikiwa ndio hasa inayojulikana, kutokana na kushiriki Ligi kuu soka Tanzania bara VPL, ambapo imekuwa ikitoa ushindani mkubwa katika Ligi hiyo.
Licha ya Mpira wa miguu, Jeshi limekuwa likishiriki Michezo mingi, na baadhi ya wachezaji wake ambao ni Askari wamekuwa vinara katika Michezo wanayoshiriki, ambapo baadhi yao wameweza kuweka rekodi kubwa za Dunia, huku wakiibuka na medali na kuandikwa katika kumbukumbu za washindi wa michezo hiyo.
Christopher Isengwe Njuguda ni mmoja Kati ya Askari waliowahi kufanya vizuri katika mchezo wa riadha ndani na nje ya nchi, ambapo aliwahi kushika nafasi ya pili katika mashindano ya Dunia ya mchezo huo (World Championship in Athletics in Helnsk) huko Finland mwaka 2005, ambapo alikimbia Mbio ndefu za kilomita 42 kwa muda wa Masaa mawili, dakika kumi na sekunde 21, na kuibuka na Medali ya Silver ambayo ni ya kwanza nchini Tanzania katika historia ya Mashindano ya Dunia.
Askari wa Jeshi la Magereza Sajenti Christopher Isengwe (mwenye bukta ya kijani) akiwa katika mashindano ya Dunia ya Riadha huko Finland mwaka 2005.
Wadau mbalimbali wamemtaja Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee kuwa ni mpenda Michezo, kwani amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA), hivyo wamekuwa na imani nae katika kuinua Michezo ndani ya Jeshi la Magereza, kwani ndiye aliye weza kuipatia Gari aina ya Costa timu ya mpira wa miguu ya Jeshi hilo Tanzania Prisons Sc mwanzoni mwa mwaka 2020, ili kuiondoa Timu hiyo katika changamoto za usafiri.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee akikabidhi kadi ya gari Aina ya Costa kwa ajili ya matumizi ya Timu ya mpira wa miguu ya Jeshi hilo, Tanzania Prisons Sc.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee, akiwasha gari Aina ya Costa Mara baada ya kulikabidhi gari hilo kwa Timu ya Tanzania Prisons Sc.
Muonekano wa Gari aina ya Costa, aliyoikabidhi Jenerali Mzee kwa Timu ya Prisons, baada ya kubadikwa Stika kuitambulisha kuwa ni gari ya Timu hiyo.
Kutokana na Jeshi la Magereza kufanya vizuri katika michezo mbalimbali, Jenerali Mzee, ameendelea kufanya Jitihada katika kuhakikisha anaboresha kitengo Cha Michezo Cha Makao makuu ya Jeshi hilo ambacho ndicho chenye dhamana ya kusimamia Michezo yote ndani ya Jeshi, hivyo ameifanyia mabadiliko ofisi hiyo, kwakupeleka safu mpya ya uongozi wenye taaluma na uzoefu mkubwa katika michezo, wakiongozwa na Mrakibu Msaidizi wa Magereza Francis Sylvester Tabu, ili kuleta matokeo chanya.
Kwa upande wake mkuu wa kitengo Cha Michezo wa Jeshi la Magereza, Mrakibu Msaidizi wa Magereza Francis Sylvester Tabu, maarufu (Farao) amesema, Wana malengo makubwa ikiwemo kuanzisha Timu ya mpira wa miguu ya Wanawake.
"Kama ofisi tuna malengo makubwa Sana, tutaanzisha Timu ya Wanawake, na hii pia hata Shirikisho la mpira TFF walituandikia barua kutushauri, lakini tunataka tuwe na Timu nzuri ya watoto wenye umri chini ya miaka 17, na kuhakikisha Timu yetu ya Tanzania Prisons Sc inapata mdhamini mkuu wa klabu ili iweze kujiendesha na kuboresha zaidi maslahi ya wachezaji wetu" alisema Farao.
Aidha Mkurugenzi wa Ufundi katika Michezo wa Jeshi la Magereza Wdr Kelvin Fredinand Tresphory, ni mmoja Kati ya wataalamu wa Michezo walio hamishiwa ofisini hapo kwaajili ya kuboresha Michezo 'Teknikale', hivyo tumefanya nae mahojiano ya kina ili kujua uzoefu wake katika Michezo, mpaka kumpelekea Mkuu wa Jeshi kumuamini na kumuweka katika nafasi kubwa inayotaka utaalamu wa Hali ya juu.
"Mimi nimesomea Michezo kwaujumla, nina Stashahada ya Elimu ya viungo katika michezo yaani (Ordinary Diploma in sports physical Education), lakini pia nina vyeti vingine vingi vya michezo mbalimbali, na nina uzoefu katika Michezo na nimeshiriki Michezo ndani na nje ya nchi, kwahiyo nashukuru Afande CGP ameniona na kuamua kunileta hapa ofisini ili kulisaidia Jeshi letu kupiga hatua katika Michezo" alisema Kelvin.
Wdr Kelvin pia ana Cheti cha wa Ualimu wa mpira wa miguu daraja la kwanza, yaani (Football coaching intermediate certificate), chini ya Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF mwaka 2018, Cheti cha mchezo wa riadha daraja la kwanza mwaka 2017, Cheti cha Ualimu na uamuzi wa mpira wa mikono(Handball intermediate certificate in coaching and Officiating), Cheti Cha Ualimu wa wavu, Cheti Cha Uamuzi wa mpira Kikapu na Cheti Cha Usemaji wa vyama na taasisi.
Wdr Kelvin Fredinand Tresphory (wakwanza Kushoto waliosimama) akiwa pamoja na washiriki wa kozi ya Usemaji wa vyama na taasisicl iliyo endeshwa na aliyekuwa msemaji mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas, uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.
Kelvin pia ameeleza kuwa amewahi kuitwa katika Timu ya Taifa ya mchezo wa Woodball Kama mchezaji na kushiriki mashindano ya kimataifa ya mchezo huo (Woodball International Championship) yaliyofanyika nchini Kenya na Uganda mwaka 2017 ambapo zilishiriki jumla ya nchi 16 na kuhudhuriwa na Rais wa mchezo huo kutoka China.
Pia amefundisha Michezo mbalimbali katika Jeshi la Magereza huko visiwa vya Shelisheli mwaka 2018 hadi mwaka 2020, hivyo amedhamiria kutua uzoefu wake kuliletea tija Jeshi la Magereza hapa nchini na kutimiza dhamira ya mkuu wa Jeshi hilo Meja Jenerali Mzee, inayo lenga kuliinua zaidi Jeshi katika nyanja ya Michezo.
"Nina majukumu na malengo makubwa tu, unajua mpaka Afande CGP ameniamini, inabidi nifanye kila niwezalo ili kuifanya Michezo inakwenda vizuri, kuzifanya timu zetu ziwe na nidhamu katika Michezo, ili ziwe bora zaidi, na nashukuru Mungu tangu niwe Technical director wa Michezo naona Mambo yameanza kwenda vizuri." Alisema Wdr Kelvin.
Anasimamia na kuuza wachezaji ndani na nje ya nchi.
Licha ya kuwa Mkurugenzi katika Michezo ndani ya Jeshi la Magereza, wdr Kelvin pia amejipambanua kuwa anajishughulisha na kusimamia na kuuza wachezaji (Sports management and Agent in football) ambapo amekuwa na wachezaji kadhaa mpaka Sasa ambao anawasimamia.
"Unajua watu wengi hawajui kama nafanya hii ishu, binafsi namsimamia Cleophace Antoni Mkandala ambaye yupo Dodoma jiji Fc, pia Rolland Narsis Msonjo ambaye nilimpeleka nje ya nchi kwenye Timu ya Independente Vellel huko Ecuador, pamoja na dogo mmoja anaitwa Baraka Sylvester anacheza timu ya Taifa ya mchezo wa Beech soccer, hawa wote ni wachezaji wangu"aliongeza wdr Kelvin.
Wdr Kelvin Fredinand (Kulia) akiwa na mchezaji Cleophace Antoni Mkandala (katikati), pamoja na Katibu wa Dodoma jiji Fc Fortunatus Johnson Mara baada ya mchezaji huyo kusaini mkataba wa kuitumikia Timu hiyo.
Kelvin amewashauri Askari pamoja na watu wote kuingia katika tasnia ya Michezo, kwani imekuwa na faida kubwa, kiuchumi hata kiafya pia, kwani Michezo kwa Sasa imekuwa ni ajira kubwa tofauti na miaka ya nyuma ambapo watu waliichukulia Michezo kuwa ni burudani tuu.
Kelvin Fredinand (Kulia) akiwa katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, akimsindikiza mchezaji anaye msimamia Rolland Msonjo, alipokuwa akielekea Ecuador katika Timu ya Independente Vellel.
Kutokana na taaluma ya Michezo na uzoefu wa viongozi wa Michezo wa Jeshi la Magereza, kumekuwa na Matumaini makubwa ya kuinuka kwa Michezo ndani ya Jeshi hilo ukizingatia Mkuu wa Jeshi, Meja Jenerali Mzee, amekuwa na dhamira ya dhati ya kulifanya Jeshi hilo kuwa Kinara katika Michezo ndani na na hata nje ya nchi.
Kwa maoni/ushauri, wasiliana na Mwandishi Geofrey Jacka. 0659794337 / 0625972465
Barua Pepe. geofreyjacka308@gmail.com
Dodoma.
No comments