}

MAGEREZA ILIVYOMTUMIA MTAALAMU BUSTANI ZA MAUA WA JESHI HILO, KUING'ARISHA MAKAO MAKUU DODOMA.

Na. Geofrey Jacka - Dodoma

Muonekano wa baadhi ya majengo ya Makao makuu ya Jeshi  la Magereza, yaliyopo Msalato Jijini Dodoma.

"Kiukweli hakuna sehemu inanishinda mimi kuotesha bustani ya Maua, hata unipeleke sehemu yenye Mwamba wa jiwe nakuoteshea vizuri tuu". Alianza kujieleza kwa tambo, mtaalamu huyo Sajenti  (SGT) Augustino Luganga, kuonesha namna anavyojiamini katika kazi yake.


Mtaalamu wa bustani za maua Sajenti Augustino Luganga akielezea namna alivyoweza kuanzisha bustani za Makao makuu ya Magereza.

Baada ya Jeshi la Magereza Tanzania kuhamia jijini Dodoma toka Dar es salaam mwezi Februari, 2020, hakuna mtu aliyeamini kama Jeshi hilo litaweza kujijengea ofisi zake za makao makuu kwa haraka, na majengo yenye ubora wa hali juu tena kwa gharama nafuu.

Lakini ilichukua takribani mwaka mmoja tuu, Jeshi la Magereza liliweza kukamilisha ujenzi huo na kuhamia katika majengo yake, huku likiwaacha wengi vinywa wazi na hata baadhi ya wakuu wa taasisi mbalimbali waliweza kufika ili kuona na kujifunza yaliyofanywa na Jeshi hilo, ambalo lilifichua siri kuwa, limetumia wataalamu wake ambao ni Maafisa na Askari pamoja na Wafungwa, katika kukamilisha shughuli zote za ujenzi.

Magereza makao Makuu jijini Dodoma.

Mtaalamu wa utengenezaji bustani Sajenti Augustino Luganga, ametusimulia mengi na kujaribu kuikumbuka safari nzima Kwaupande wake, huku akisisitiza kwakusema "Ndugu yangu mwandishi, ungepaona hapa palivyokuwa mwanzo, usingeamini kama pangebadilika na kuwa Kama Eden leo hii, hapa palikuwa Jangwa".

Muonekano wa sasa wa bustani iliyoanzishwa na kusimamiwa na mtaalamu Luganga.

Luganga ni askari na mmoja kati ya wataalmu wa Jeshi la Magereza, mwenye cheo cha Sajenti (SGT) ambapo alitudokeza kuwa, alifika Dodoma kwa uhamisho kama ulivyo utaratibu wa kawaida wa uhamisho kwa mahitaji ya kazi, akitokea mkoani Morogoro ambako alikuwa anafanya kazi za uaskari kwa kadri ya mpangilio wa kazi za Gerezani.

"Hapa nimehamishiwa mwaka jana 2020, nilikuwa Morogoro, Gereza moja linaitwa Idete kama ushawahi kulisikia, lakini kabla ya hapo nilitokea pale Morogoro mjini, hivyo nakumbuka hapa nilianza kazi mwezi wa Saba tarehe 17 kama sijakosea" alisema Luganga

Aliendelea kuelezea ugumu alioupata mwanzoni ni ukame wa eneo husika pamoja na eneo kutofanyiwa "Land scaping" hivyo ilibidi ndio viwe vitu vyakuanza navyo kuvitatua ili shughuli nyingine zifuate.

"Eneo lilikuwa ni kame sana, pia halikufanyiwa land scaping,  hivyo nilianza zoezi la kusawazisha eneo ili level (sawa) na pia niligundua udongo wa hapa hautanifaa, nikashauri tukasombe kifusi mahali ambapo niliona udongo mzuri, hivyo vitu vilifanyika fasta sana kwasababu vitendea kazi vilikuwepo" alieleza Luganga.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo alisema kuwa kuna aina  tatu za bustani ambazo ni Uniformity garden, yaani bustaani yenye aina moja ya maua, VIP garden, ni zile bustani zenye maua tofauti tofauti na adimu, na Bush garden, ambazo zenyewe ndani yake kuna mchanganyiko wa matunda mbalimbali, ambazo zote ameweza kuzitengeneza katika eneo la Makao makuu ya Magereza.

"Hapa nimepanda aina zote hizo nilizotaja, na utaona pale bush garden, ambayo hii ina mkusanyiko wa matunda, miwa, mapapai, zabibu, yani ipo vizuri sana, na hapo hapo katikati ya bustani kunakuwa na sehemu maalumu ambayo ni very classic kwaajili ya bosi kupumzika nakupata bidhaa za matunda kutoka hapohapo bustani, anakula kitu freshi kabisa, lakini hili eneo kwasasa bado halijakamilika ila bustani yenyewe tayari ipo" aliongeza mtaalamu.

Eneo la bush garden ambalo lina maua pamoja na mkusanyiko wa matunda mbalimbali.

Kuhusu aina za maua alizopanda Luganga alisema, zipo aina nne, Croton, Palm, Shirabs na Ukoka yaani green carpet, ambazo aina zote hizo pia zimegawanyika katika sehemu nyingi, kama palm ambayo inafanana na mnazi ina Royal palm, American palm, sugu palm, Golden palm na Tanga palm, huku aina ya Shirabs ikiwa na Orianta ambayo asili yake ni mikoa ya Morogoro, Arusha na Tanga, huku akilitaja ua aina ya Infobia au Jesus nalo likiwa katika aina hii ya Shirabs.

Ua Aina ya Infobia au maarufu Kama Jesus, ambalo lipo katika kundi la Shirabs.

Aidha mtaalamu alieza pia changamoto ya wadudu kushambulia Sana maua, hivyo amesisitizia matumizi ya dawa za kuulia wadudu ili kuhakikisha bustani haiharibiwi huku akiweka wazi mambo mambo yakuzingatia kabla ya kuanzisha bustani kuwa ni pamoja na aina ya udongo, mbolea pamoja na maji ya uhakika kwaajili ya kumwagilia.

"Maua pia yanashambuliwa sana na wadudu kama nyuki, mchwa, kuna  wadudu wanaitwa infectory, na hata mbu, kwakuwa tunamwagilia sana maji hivyo pia mbu huzaliana, kwaiyo lazima tufanye furmigation, na kuna dawa kama Navas pamoja na terminate killer kwaajili ya mchwa" alisema Luganga.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee (katikati) akikagua bustani, eneo la bush garden lenye maua na matunda.

Kwaupande wa gharama za kuanzisha bustani Luganga alisema, inategemea na aina ya bustani unayotaka kuianzisha pamoja ukubwa wa eneo unalolitaka, huku akitoa ushauri kwa watu wa kipato cha kawaida watumie aina ya bustani yenye aina moja ya Maua (Uniformity garden), kwani gharama zake zipo chini kidogo.

Ukiachana na Maua, Luganga pia ni mtaalamu wa kudizaini wanyama mbalimbali kwaajili ya mapambo, milima ya bustanini na maumbo mengine tofauti, huku akiweka wazi kuwa amemshauri Kamishna Jenerali kuwa wanaweza kuandaa uwanja bora kabisa wa mchezo wa mpira wa miguu kwani anao uwezo wakuandaa vizuri eneo la kuchezea (Pitch) ukizingatia vifaa vyote vipo ikiwemo Escavetor.

Kuhusu faida za bustani mtaalamu amesema kuwa ni pamoja maua mengi kutumika kama dawa, lakini amesema kuwa kupitia bustani hii wanaweza kuwauzia watu wengine aina mbalimbali za maua, huku akiweka wazi kuwa kiloba kimoja cha ukoka kinauzwa kati ya shilingi elfu 25 mpaka 30.

Pia kupitia bustani hii Jeshi limeweza kujitangaza na kupelekea kupata tenda kwenye taasisi nyingine ikiwepo ofisi za Polisi makao makuu, pamoja na Ofisi za Shirika la utangazaji Tanzania (TBC), ambapo mkuregenzi wa shirika hilo alitembelea Magereza makao makuu ili kuona na kujifunza kilichofanywa na Wataalamu wa Magereza.


Mkurugenzi mkuu wa shirika la utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayoub Rioba (katikati), alipotembelea Makao makuu ya Jeshi la Magereza, kwa lengo la kujifunza.

Luganga pia amewahi kufanya shughuli za bustani katika maeneo mbalimbali ikiwemo Magereza mkoa Morogoro, viwanja vya nanenane Morogoro, Gloness Hotel, Morogoro na Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya mkoa wa Morogoro.

Kwa hakika Jeshi la Magereza limejawa na wataalamu wa kila fani, na Sajenti Augustino Luganga ni ushahidi tosha wa jambo hili, na endapo wataalamu watatumiwa vizuri kulingana na taaluma zao Jeshi litapiga hatua kubwa sana katika maendeleo.

Hongera sana Kamishna Jenerali kwa kuthamini wataalamu, na hongera sana kwa mtaalamu Luganga kwa kuing'arisha Makao makuu ya Magereza jijini Dodoma.

Kwa maoni/ushauri, wasiliana na mwandishi Geofrey Jacka. 0659794337 / 0625972465 geofreyjacka308@gmail.com

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.