}

Kazenga amezipongeza timu za sekta yake kufanya vyema kwenye mashindano ya Kombe la Mei Mosi



Na Bahati Mollel-TAA, Iringa
WAKATI Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Bi. Easter Kazenga amezipongeza timu za sekta hiyo kwa kufanya vyema kwenye mashindano ya Kombe la Mei Mosi inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Iringa, jana kwenye uwanja wa Samora timu ya soka iliwachapa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa bao 1-0.

Bi. Kazenga amezipongeza timu za michezo ya kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume, soka, netiboli, karata, bao, draft, riadha na baiskeli za Uchukuzi baada ya kuwatembelea kwenye kambi yao mara baada ya kumalizika kwa michezo.

“Ninawapongezeni sana kwa kufanya vizuri katika michezo hii, nimekuja kuungana nanyi ili kuwatia moyo na nitakuwa hapa kwa siku kadhaa na baadaye Katibu Mkuu na wengine watakuja, hivyo tuendeleze ushindi na tuchukue vikombe vyote vya ubingwa,” amesema Bi. Kazenga.

Hatahivyo, amewasisitizia wachezaji hao kuwa na nidhamu wawapo ndani na nje ya kiwanja ili kujenga sifa nzuri ya sekta hiyo.

Uchukuzi SC inayoundwa na wachezaji wazoefu akiwemo aliyewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Eliutely Mholeli alipata bao lake pekee kwa njia ya penati iliyofungwa na Mahamudu Khamis katika dakika ya 52 baada ya Sigfrid Kikoti kuchezewa rafu na Joseph Mlimi wa TRA.

Hatahivyo, wachezaji wa pande zote mbili walishindwa kuonesha mchezo mzuri kutokana na kucheza huku mvua ikinyesha na uwanja kujaa maji katika baadhi ya sehemu na kusababisha wachezaji kuanguka hovyo huku mpira ukikwama katika madimbwi.

Katika mchezo wa netiboli uliochezwa kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUKU), timu ya Uchukuzi iliwaadhibu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuwafunga magoli 38-13.

Uchukuzi SC inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa na Bandari, Judith Ilunda ilikwenda mapumziko wakiwa na magoli 15-7, ambapo hadi mwisho wa mchezo mfungaji wake Matalena Mhagama alifunga magoli 28 na Bahati Herman magoli 10, wakati wa Tanesco Tina Mbuisa magoli tisa na Caltace Manapo magoli manne.

Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya Msingi Mlandege, mabingwa watetezi timu ya Uchukuzi iliwavuta Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa mivuto 2-0.

Kwa upande wa wanaume mabingwa watetezi Uchukuzi waliwapeleka puta Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwavuta mivuto 2-0.

Michuano hiyo itaendelea leo kwa mechi za soka kati ya NAO dhidi ya GGM, wakati katika netiboli watacheza RAS Iringa na Hifadhi ya Ngorongoro.
MWISHO
 
 Kipa Frank Mvula wa timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akiwa ameshindwa kucheza mpira wa penati uliopigwa na Mahamudu Khamis wa Uchukuzi katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Samora. Uchukuzi walishinda bao 1-0. (Picha na Bahati Mollel-TAA).












No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.