}

WABUNGE NANE WAREJESHEWA UANACHAMA CUF

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo Ijumaa Machi 16 imewarejeshea uanachama wa CUF, Wabunge nane waliovuliwa uanachama mwaka jana na Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof. Ibrahim Lipumba, hadi pale kesi yao ya msingi Na. 143/17 waliyoifungua mahakamani hapo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji wa Mahakama Kuu, Lugano Mwandambo mbele ya Msajili wa Mahakama hiyo, baada ya kutolewa hukumu ya shauri dogo Na. 479/2017 ambayo iliwarejeshea uanachama wabunge hao na madiwani wawili pamoja na kuzuia mamlaka zote za CUF na taasisi nyingine kujadili juu ya uanachama wao.

Hoja zilizotumiwa katika kutolewa hukumu hiyo ni pamoja na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lililotumika kuwavua uanachama kudaiwa siyo mamlaka ya mwisho ya nidhamu kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, ambapo wabunge hao walikata rufaa kwenye mamlaka ya juu zaidi ambayo ni Mkutano Mkuu wa Taifa CUF. 

Ya pili, ni lengo la kuhifadhi hali iliyokuwepo “Maintanance of Status Quo” ili kulinda haki za muombaji na kuepusha athari pale itakapobainika kuwa haki ilistahili kuwa upande wake mwisho wa shauri la Msingi. Na kwamba Mahakama Kuu ilishawahi kufanya hivyo kwa mashauri kadhaa na ni haki ya kisheria pale Mahakama itakapoona haja na kuzingatia hoja za msingi zilizotolewa na waombaji husika.

Hoja ya mwisho iliyotumiwa katika kutoa uamuzi huo, ni uwepo wa mashauri mengine Mahakamani hapo yanayohoji juu ya uhalali wa uongozi au vyombo vya maamuzi ndani ya CUF ikiwemo uhalali wa uenyekiti wa Prof. Lipumba.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.