Wachezaji Simba wanafahamu thamani na uzito wa jezi wanazovaa?
ABDUL MKEYENGE
LEO wacha nimtafune jongoo mbichi, bila kujali ukakasi nitakaoupata katika kinywa. Nina marafiki wengi ambao ni wachezaji wa Simba.
Wao wananiheshimu kama Mwandishi nami nawaheshimu kama wachezaji. Lakini leo nimeamua kumtafuna jongoo, si vinginenyo.
Simba imeshatua zake Dar es Salaam ikitokea Zanzibar kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi. Imetua mchana wa leo vichwa vya wachezaji vikitazama chini, wengine waliweka earphone masikioni na wengine wakivaa kapelo kubwa kwa ajili ya kujificha nyuso. Hivi leo hii tushindwe kumjua mchezaji wa Simba kwa kujibadili muonekano? Simba imerudi na muonekano huo.
Hawana wa kumlaumu, walaumiwe wachezaji. Nimeitazama Simba katika michezo yake mingi msimu huu. Wana kila kitu, lakini wanakosa mapambano. Mpira ni mchezo wa mapambano kwa wanaume 22 kupambana uwanjani. Ajabu iliyoje wachezaji wa Simba hawataki kupambana. Shida yote hii inaanzia kwao.
Joseph Omog ameondoka kwa ajili ya wachezaji. Viongozi wa Simba wasipokuwa makini Masoud Djuma nae ataondoka kwa ajili ya wachezaji. Timu inacheza 'kifather ' sana. Ni ngumu kupata mafanikio katika hali hii.
Leo Omog hayuko Simba, lakini Simba imeonekana kuwa ile ile kama ya Omog. Hivi naweza kupata majibu nikiuliza tofauti ya Simba ya Omog na Simba hii ya Djuma? Timu inacheza kivivu. Wachezaji wanacheza ni kama wana kazi zao nyingine zinazowalipa mishahara minono na wako Simba kwa ajili ya kupasha moto miili kwa ajili ya kujiweka vizuri na chakula cha jioni.
Sio utani au najisifu, Simba hii ya kivivu mimi Abdul Mshindo Mkeyenge na kitambi changu naweza kucheza vyema na nikawa staa kama walivyo mastaa wachezaji wengine. Rekodi zangu mwanana anazo kaka yangu Said Lukoo, mtafuteni awape.
Niliwahi kuwaona mashabiki wa Simba wakifurahia baada ya timu yao kupata kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya TP Mazembe Uwanja Taifa. Mashabiki wale hawajafurahia kufungwa, walifurahia jinsi timu yao ilivyopambana kiume uwanjani, licha ya kufungwa. Ni lini Simba hii itarudi tena?
Nilidhani spirit walioionyesha Wazanzibar kwenye michuano ya Chalenji ingewangia wachezaji wa Simba ambao siku hizi wanacheza kama timu ya watoto wadogo chini ya miaka 12 wanaojifundisha soka.
Yote tisa, kumi wachezaji wa Simba wanafahamu thamani na uzito wa jezi wanazovaa? Hapa panahitaji uzito kidogo. Kwa pamoja tushushe pumzi zetu kwanza!
Simba ni timu kubwa. Wachezaji wake wanalijua hili? Simba ni miongoni mwa timu zenye mashabiki wengi Afrika, wachezaji wake wanalijua hili? Wachezaji wanafahamu kuwa kuna watu wamepoteza maisha yao na watu wengine kufilisika kisa Simba?
Mpaka leo hii Simba imesimama na inaitwa Simba na inasajili wachezaji wa gharama kubwa na kuwalipa mishahara minono. Wachezaji wake wanalijua hili? Wanajua ilikotokea klabu?
Inawezekana yote haya yanatokea kutokana na wachezaji kutoambiwa maana ya mchezaji wa Simba na kuvaa jezi za Simba. Hili ni jambo muhimu ambalo huenda viongozi hawajawaambia wachezaji walipokuwa wakipeana mikataba. Inawezekana viongozi na mchezaji waliishia kupeana mikataba kisha wakapiga picha ya pamoja, huku sura zao zikijaa bashasha. Inawezekana.
Nafahamu mpira kuwa na matokeo matatu. Kushinda, kufungwa na kupata sare. Na haijawahi kuandikwa popote pale kuwa Simba inapocheza ni lazima ishinde, isifungwe wala kupata sare, lakini ni kweli wachezaji wa Simba wamewafanyia fair mashabiki wao dhidi ya Green Warrios ya rafiki yangu Azish Kondo? Mzaramo kalonga Zua Diswa.
No comments