}

KOCHA MBEYA CTY AFUNGIWA, VILABU LIGI KUU VYAPIGWA FAINI

Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani katika mechi namba 95 dhidi ya Kagera Sugar iliyomalizika kwa sare ya 1-1 Januari 1, 2018 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. 

Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu na Kamati iliiagiza Sekretarieti ya Bodi ya Ligi kutoa waraka kwa wamiliki wa viwanja kuhakikisha timu zinaingia uwanjani kwa kutumia milango rasmi tu.

Kocha wa Mbeya City, Mrundi Ramadhani Nswazurimo amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la kumkashifu mwamuzi Israel Mujuni Nkongo katika mechi namba 100 dhidi ya Tanzania Prisons ambayo timu yake ilichapwa 3-2.  
Adhabu ambayo imezingatia Kanuni ya 40(11) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.

Kocha Mwazurimo aliondolewa kwenye benchi (ordered off) na Mwamuzi baada ya kumtolea lugha ya kashfa katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 14, 2018 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.


Mbeya City nayo imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwa madai alikataa kutoa penalti kwa timu hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.


Kamati imeteua wajumbe watatu kupitia mkanda wa mechi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine itachunguza kiwango cha uchezeshaji cha Mwamuzi wa mechi hiyo, Bw. Israel Nkongo na kuwasilisha taarifa yake kwa ajili ya hatua zaidi.


Azam FC imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na kukataa wachezaji wake wakaguliwe ndani kwenye mechi namba 103 dhidi ya wenyeji Majimaji iliyomalizika kwa sare ya 1-1 Januari 18, Uwanja wa Majimaji mjini Songea kwa madai kuwa chumba kimepuliziwa dawa.


Kitendo cha timu hiyo ni kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi yao imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu. Pia klabu hiyo imeandikiwa barua ya kutakiwa kuthibitisha madai yake kuwa chumba hicho kilikuwa kimepuliziwa dawa.


Mtunza Vifaa wa Singida United FC, Mussa Rajab amefungiwa mwezi mmoja na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuingia uwanjani wakati wa mapumziko kumlalamikia mwamuzi katika mechi namba 104 dhidi ya wenyeji, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Kitendo alichofanya Mtunza Vifaa huyo katika mechi hiyo iliyochezwa Januari 18, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kimekiuka Kanuni ya 14(10) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 41(2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Viongozi.


Stand United imepewa onyo kali kutokana na timu yake kuchelewa kwa dakika sita kwenye kikao cha maandalizi ya mechi na pia kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika tisa katika mechi namba 106 dhidi ya wenyeji Mbao FC timu hiyo ya Shinyanga ikishinda 1-0 Januari 20  Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.


Adhabu kwa klabu hiyo iliyokiuka Kanuni ya 14(2a) ya Ligi Kuu, imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.