}

KOCHA MKUU KILIMANJARO STARS AJIPANGA KUIBA SIRI YA ZANZIBAR HEROES.

Kocha Mkuu wa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje amepanga kesho Jumanne Desemba 5, 2017 kuanza kufanyia kazi upungufu ulioonekana kwenye mchezo dhidi ya Libya  uliofanyika Jumapili Desemba 3, mwaka huu.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kenyatta ulioko Machakos hapa nchini Kenya, Tanzania Bara ilipata sare katika safari ya kuwania Kombe la Cecafa – michuano inayofanyika hapa Kenya.

Ninje amesema katika mchezo huo wa kwanza waliecheza katika kiwango cha kuridhisha na kikubwa anataka kuangalia namna ya kufanyia kazi upungufu ikiwa ni pamoja na pale timu inapopoteza mpira.

Anasema kwenye mchezo dhidi ya Libya timu ilicheza kuanzia nyuma kupitia sehemu ya kiungo na kuunganisha sehemu ya ushambuliaji – jambo ambalo limemfurahisha kwa namna timu ilivyotengeneza nafasi.

Akizungumzia mchezo unaofuata dhidi ya Zanzibar Heroes, Ninje amesema ni mchezo mgumu kama ambavyo historia inaonesha wakati timu hizo mbili zinapokutana.

“Lakini kuanzia mazoezi ya kesho nitaiandaa timu kupata ushindi na nimepanga kwenda kuitazama Zanzibar itakapocheza mchezo wake wa kesho dhidi ya Rwanda,” amesema.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.