}

AZAM KWENDA MAPINDUZI KESHO KUTWA

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, sasa inatarajia kufungua pazia la michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kumenyana na Mwenge ya Pemba Jumapili hii saa 10.30 jioni.
Kwa mujibu wa ratiba ya awali ya michuano hiyo kabla ya kubadilishwa, ilionyesha kuwa Azam FC ambayo ndiyo bingwa mtetezi ikiwa Kundi A, itacheza na Jamhuri ya huko Januari 2 mwakani.
Kutokana na mabadiliko hayo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam keshokutwa Jumamosi kuelekea Visiwani Zanzibar tayari kushiriki michuano hiyo inayoyarajia kufikia tamati Januari 13 kwa mchezo wa fainali kupigwa.
Mara baada ya mchezo huo wa awali, Azam FC  itashuka tena dimbani kwa mchezo wa pili dhidi ya Jamhuri utakaofanyika Januari 3 saa 10.30 jioni.
Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, watacheza mchezo wa tatu wa hatua ya makundi dhidi ya URA ya Uganda utakaofanyika Januari 5 saa 10.30 jioni, ambapo itamalizia raundi ya mwisho ya makundi kwa kumenyana na Simba Januari 6 saa 2.15 usiku.
Azam FC ikisonga kwa hatua ya nusu fainali, mechi yake itapigwa Januari 10 siku ya mechi ya hatua hiyo huku fainali ikitarajia kupigwa Januari 13, mechi zote zikifanyika Uwanja wa Amaan, Unguja, Zanzibar.
Mwaka huu Azam FC ilitwaa taji hilo baada ya kuifunga Simba bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali, lililofungwa na nahodha wake Himid Mao ‘Ninja’, kwa shuti kali la umbali wa takribani mita 30 lilimshinda aliyekuwa kipa wa wekundu hao, Daniel Agyei.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.