}

NAIBU WAZIRI WA KILIMO AUNGURUMA MTWARA KUHUSU VYAMA VYA USHIRIKA.

Na Mathias Canal, Mtwara.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Machuche Mwanjelwa leo Novemba 18, 2017 amemuagiza Mrajisi wa vyama vya ushirika kukamilisha haraka kazi ya uchunguzi kwenye Bodi za vyama vya ushirika vya Mkoa wa Mtwara ili kubaini sababu zilizopelekea kuuzwa kwa magunia kiholela.

Alisema kuwa kumalizika kwa uchunguzi huo kutarahisisha kuchukuliwa haraka hatua kali za kisheri kwa wale wote watakaobainika kukiuka sheria No 17 ya vyama vya ushirika.

Naibu waziri alitoa agizo hilo wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji na kata ya Chiungutwa, Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara mara baada ya kugundua kuwa kuna viashiria vya ukiukwaji wa taratibu katika upatikanaji wa magunia ya kuhifadhia korosho wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani humo.

Sambamba na hilo Naibu waziri Mhe Mwanjelwa wakati wote wa mkutano huo ameshuhudia malalamiko kutoka kwa wakulima wa zao la korosho wa Chama cha Ushirika cha Masasi-Mtwara Cooperative Union Ltd (MAMCU) kuhusu ucheleweshwaji wa upatikanaji wa maguni kutoka kwa mzabui, Mapungufu ya kilo kati ya PDA na WHRs ghala kuu, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa malipo ya wakulima kwa njia ya benki kutoka kwa wanunuzi.

Katika ziara yake hiyo kilio cha wananchi wengi na wakulima walisiitiza zaidi kuhusu kukosekana kwa magunia hayo huku wakieleza kuwa wakati mwingine kuchelea kufika ama kutowafikia kabisa jambo ambalo linachangia kupunguza thamani ya zao la korosho.

“Nataka Mrajisi ufanye na ukamilishe kazi yako ya uchunguzi na baada ya kuipata taarifa hiyo hatua stahiki zitachukuliwa kwa wale wote watakaogundulika kukiuka sheria ya nchi” Amekaririwa Naibu Waziri Mhe Mwanjelwa

Mbali na agizo hilo Naibu Waziri pamoja na wabunge wa Mkoa wa Mtwara walipata nafasi ya kujionea mnada wa tano wa ununuzi wa korosho unavyoendelea.

Hata hivyo Mnada wa tano ulishuhudiwa Kilogramu 7,524,104 za korosho zikiuzwa kwa thamani ya zaidi ya Bilioni 30.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mhe Mwanjelwa amesema Wizara itayafanyia kazi haraka mapendekezo ya tume iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe Gelasius Gasper Byakanwa kufanya uchunguzi kuhusu mwenendo mzima wa magunia pamoja na upatikanaji wake.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.