}

MKEYENGE; HUYU SIO AJIBU NINAYEMFAHAMU


MAKALA YA ABDUL MKEYENGE

SWAHIBA wangu Ibrahim Ajib yuko kwenye kilele cha ubora wakati huu. Ndani ya muda mfupi na Yanga amegeuka mchezaji muhimu kwenye kikosi. Anafanya kazi inayomvutia kila mmoja. Huyu ndio Ajib.
Mara zote nilitamani Ajib afanye hiki anachokifanya sasa, sababu nazijua mwenyewe na sihitaji niziweke hapa. Kutoka chini ya moyo wangu nafurahia sana maendeleo yake.
Nafahamu kila kitu kuhusu yeye na maisha ya alikotoka, si vyema leo tukianza kufukua makaburi ambayo hayatasaidia kitu zaidi yataniharibia mimi na yatamuongezea chuki. Kwanini tufike kote huko?
Leo nimekuja hapa na kitu kimoja tu! Kitu chenyewe kinaitwa huyu sio Ajib ninayemfahamu. Ni hiki na sio kitu kingine.
Zikiwa zimesalia siku tatu kushuhudia mchezo wa watani wa jadi, Ajib ni mchezaji anayepandisha na kushusha presha za watu wa upande wa pili, japo wenyewe ukiwauliza wanakuwa wazito kuikiri presha waliyonayo.
Kuna sababu mbili za msingi zinazofanya Ajib atazamwe kwa jicho la kihafidhina. Mosi ni huu ubora ulioimarika maradufu, pili ni kwanini Ajib awe mahiri kiasi hiki wakati miezi sita iliyopita alikuwa mchezaji anayeweza kukaa benchi na watu wasishituke. Haya mambo mawili yanawachanganya sana watu.
Kama ubora huu angekuwa nao Obrey Chirwa, Donald Ngoma, tusingeshituka, lakini kuwa nao Ajib ni pigo la kimya kimya linalowawewesesha watu. Nani anayefurahia maendeleo ya kijana huyu? Ni watu wachache, lakini wale mashabiki wenzangu oya oya si wazito kutokeza hadharani na kusema Ajib hana madhara kwao na hajui mpira.
Binafsi sikutaraji kama Ajib atakuwa hivi ndani ya Yanga, nilimbeza. Lakini kwa anachokifanya sasa ni kheri kwake na familia yake. Wakati mwingine kuheshimu taaluma ya mtu ni kitu kizuri.
Ajib amekuwa hivi sasa. Anacheza mpira wa kiutu uzima. Huyu si Ajib yule aliyekuwa anakaa na mpira muda mrefu bila sababu za msingi mpaka kupokonywa na jukwaa kumtusi. Huyu wa sasa yuko committed uwanjani.
Nadhani msimu huu ukiisha anapaswa kutazama na nje. Inachosha sasa kuona Msuva akicheza Morroco, Ajib akicheza Tanzania. Inatosha sasa. Msuva ni hatari kama ilivyo kwa Ajib, lakini Ajib ana kipaji maridhawa.
Nasikia kuna mazoezi ya ziada ameyaongeza kuyafanya na ndiyo yanayoleta makelele yote ya mjini hivi sasa. Mwisho wa makelele haya ni kwenye uvungu wa miguu yake October 28, uwanja wa Uhuru. Hapa tutapata test sahihi ya ubora wake.
Wasiwasi wangu kwa Ajib unabaki sehemu moja tu. Hana bahati na michezo mikubwa. Ni mchezo mkubwa mmoja tu aliyocheza kwenye kiwango chake, ni mchezo wa Simba dhidi ya Azam uliomalizika kwa sare ya 2-2, Ajib alifunga mabao yote, lakini michezo yote mingine huwa anadhurura uwanjani.
Historia zimewekwa ili zivunjwe. Kuna kitu nakiona Ajib anaenda kukifanya uwanjani Jumamosi, bila kujali timu yake itashinda, itapata sare au itafungwa.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.