}

MASAU AIPA EKO AZAM KUTWAA KIKOMBE CHA MAPINDUZI



Kama ni jeshi ninyi ni lile la Umoja wa Mataifa linalopambana kuleta amani ndani ya Mataifa yasiyo na amani!

Amani ilitoweka ghafla katika miji, vitongoji na vijiji! Watu walilazimika kutembea kwa tahadhari, makundimakundi, wenye hofu na mashaka mengi juu ya maisha yao, walilala mapema, kisa na mkasa makelele ya mnyama aliyeishiwa mbinu za uwindani, badala yake sasa, anaparamia wanyama waliochoka na mizoga!

Mnyama huyo mchosho kwa sasa, akibahatika kukutana na kiumbe kilichojifia au kisicho na nguvu za kutosha, kidhaifu na kujikamatia tayari kwa mlo, hupiga kelele balaa, makelele ya kuogofya ambayo, huogofya mpaka watu kwenye kakazi!

Lakini akipata msosi wa ubwete kiasi hicho, anajisahau kuwa shibe hiyo si ya kudumu milele, bado anahitaji mlo ili maisha yaende atapiga kelele huyo kiasi cha kuwafanya wanyama anao walenga kuwala kuchukua tahadhari ya kukabiliana naye!

Ajabu kweli mnyama wewe! Hujamkamata mnyama, unapiga makelele pori zima kwa furaha eti, kufurahia nyama ya mnyama ambaye hujamkamata, mwenye nguvu, maarifa na uwezo wa kukushinda? Ona ulivyoumbuka na kudharirika ndani ya mbuga changa ya Chamazi, yenye mnyama huyo hatari anayekuzidi kila kitu! Sina sababu ya kukupa pole maana uliyataka mwenyewe!

Mtoto ukimpa wembe alioulilia, ukimkata ukaanza kumuhurumia utaonekana chizi kwa wenye utimamu wao! Akilia kwa kukatwa na wembe alioulilia, wewe uliyempa ni kucheka na kufurahia hata kimoyomoyo kwamba, wembe umefanya kazi iliyokuwa ya lazima kuifanya, umekata tayari, kilichopo ni mtoto kuhangaika na maumivu, atakoma siku nyingine hawezi kupiga makelele kulilia vitu vya hatari kama wembe uliomtoa damu tayari!

Huyu mnyama, nadhani atakoma kupiga makelele kufurahia kula nyama ya mnyama ambaye hujamkamata wakati akijua ujanja na uwezo wa kumkamata hana! Nahisi asipo koma, akaendelea na hayo makelele yake, kuna hatari ya kufa njaa, huyo mnyama mwingine anayemnyemelea, atamkosa, ataliwa na wanyama wengine wanaopatikana mbuga kama zile za Mabatini, Chamazi, Manungu, wenye nguvu, mwendo wao wa kimya kimya mawindoni! Hata yule wa Jangwani japo naye kachokachoka hivi, anaweza akajikongoja akamnyang'anya mnyama, mnyama anayempigia chapuo!

Mnyama bana, anajua kabisa yule mnyama wa Jangwani pale ilikuwa bahati tu kumla lakini, khaaaaaa, watu walikosa amani na raha, wengine walizirahi tu kwa makelele yake, sijui angefanikiwa kumla na huyu wa Chamazi ingekuwaje! Wengi wangekufa, maana makelele yake yangetisha zaidi! Mnyama chali, mji umetulia, kimyaaaa kama maiti ndani ya jeneza inayosafirishwa kwa usafiri wa jahazi ndani ya bahari iliyochafuka!

Hongereni sana Azam kwa ubingwa wa kombe la Mapinduzi mwaka 2017, mlistahili!

Hiyo ndiyo Azamu, siyo mimi tu bali Watanzania wengi wanayoidhani iwe hivyo!

Kama ni ukubwa, Azam ninyi ndio wakubwa wa soka la nchi hii, hao wengine ni mbwembwe tu, hawana ukubwa wowote zaidi ya ukongwe wao!

Wote mlioshiriki mashindano hayo ya Mapinduzi, niwapongeze kwa ushiriki wenu, bila ninyi mvuto na msisimko kwenye hayo mashindano usingekuwepo!

Njoni sasa tukabane huku kwetu, kila mmoja kwa uwezo wake awanie hiki kitumbua! Ni vita kwani, tupo wengi tunaokihitaji! Tukiwanie kistaarabu, tabia za ajabu ajabu, zinaweza ndiyo kukusaidia kukipata kitumbua hiki, lakini huko mbele ya safari, utaumbuka! Utavembelwa tu, kwani ulikifukamia kitumbua pasipo na uwezo wa tumbo matokeo yake inakuwa aibu mbele ya wanaume waliojiandaa!

Hakika, kutesa kwa zamu! Ukitesa leo furahi, kesho usinune, mfurahie tu atakayetesa maana imeandikwa, "Kutesa kwa zamu"!

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.