}

Baada ya ushindi wa Simba dhidi ya Ruvu shooting, Masau bwire atoa waraka mzito, waamuzi hawapo salama.



Mapambano mkali kati ya Simba na Ruvu Shooting uliofanyika uwanja wa Taifa, Dar es salaam Desemba 29, 2016 uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 umeacha maulizo mengi kwa Wadau, wapenzi na washabiki wa soka la Tanzania.

Miongoni mwa maulizo hayo ni maamuzi ya mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza, uchezaji wa winga ya kulia wa timu ya Ruvu Shooting Jabir Aziz Stima na Rungu la Masau Bwire!

Mwamuzi Mahagi mbali na kulalamikiwa na uongozi wa Ruvu Shooting, Wadau wa soka la Tanzania walioshuhudia mtanange huo na uchezeshaji wa mwamuzi huyo pia wamemlalamikia kwa kuonesha udhaifu mkubwa katika kuzitafsiri sheria 17 za mpira wa miguu akielezwa kutoa upendeleo kwa Klabu ya Simba ili ipate matokeo Chanya!

Yapo matukio kadhaa ambayo yanaweza kushahidisha malalamiko hayo ya Ruvu Shooting na Wadau wa soka dhidi ya maamuzi ya upendeleo ya mwamuzi Mahagi katika mchezo huo, mojawapo ikiwa ni adhabu aliyoitoa dakika ya 27 ambapo mashambulizi wa Simba alinyang'anywa mpira miguuni na beki wa Ruvu Shooting nje kidogo ya 18 bila hata kugusana! Washabiki walipiga kelele kutolewa kwa adhabu hiyo ambayo waliiona haikuwa sahihi kutolewa!

Dakika ya 41, wachezaji wawili pinzani waliruka kuupiga kichwa mpira wa juu, kawaida wachezaji wanapokwenda juu kuutafuta mpira wa juu kwa kichwa, lazima tu watagusana kwani mpira wa miguu kugusana hakuepukiki, ni mchezo wa kugusana lakini ajabu walipofika tu chini, faulo kuelekea Ruvu Shooting. Hapa pia washabiki walipiga kelele kuonesha adhabu hiyo "mbeleko".

Dakika ya 43 Mahagi alitoa kadi ya njano kwa kipa wa Ruvu Shooting kwa madai ya kuchelewesha mpira alipoupiga nje mpira mmoja kati ya miwili iliyokuwa ndani ya uwanja. Kila mmoja hapa ukiacha upande uliokuwa ukinufaika na maamuzi hayo aliona dhahili kabisa kipa Bidii Hussein kapewa kadi hiyo kimakosa! Mahagi hapa alitakaje, kipa apige mpira mmoja uwe mchezoni ndipo aupige wa pili kuitoa nje? Sheria na kanuni za mchezo wa mpira wa miguu Tanzania zinasemaje katika hili? Mnaofahamu zaidi labda mnisaidie, inakuaje hapo!

Dakika ya 44, mashambulizi wa Ruvu Shooting alichomoka mbio kutoka katikati ya wachezaji wa Simba kuuwahi mpira uliopigwa upande wa Mashariki mwa lango la Kusini, lakini mwamuzi Mahagi kwa usaidi wa line 1, Ferdinand Chacha naye kutoka Mwanza alipiga filimbi kwamba mchezaji huyo tayari alikuwa katika nafasi ya kuotea!

Dakika ya 87, mshambulizi wa Ruvu Shooting alikamatwa na kuvutwa na mchezaji wa Simba hadi kuangushwa chini na kufanikiwa kumnyang'anya mpira lakini mwamuzi Mahagi hakutoa adhabu yoyote, "Kapeta" wanajisemea vijana wa kizazi hiki!

Hayo ni machache kati ya mengi aliyoyafanya Mahagi yaliyoonekana kwa kadamnasi kwamba alilenga kuuhumiza upande mmoja na kuunufaisha upande mwingine kwa sababu anazozijua yeye!

Kunya ni Bata, akinya Kuku ni Sehemu ya starehe

Baada ya dakika 90 za mchezo huo, uongozi wa Ruvu Shooting ulizungumzia mapungufu waliyoyaona katika mchezo huo ikiwa ni pamoja na yale ya kimaamuzi lakini pia mapungufu kwa baadhi ya wachezaji wake hasa Jabir Aziz Stima ambaye katika mchezo huo alionekana kutokuwa katika kiwango chake cha kawaida!

Jabir Azizi alipokea mpira akiwa ndani ya 18, peke yake, akitazamana na kipa wa Simba Daniel Agyei,  alifanya kile ambacho kilimshangaza kila mmoja uwanjani kwani, alikuwa na asilimia 99.9 kufunga goli lakini yeye badala ya kupiga mpira kuelekea langoni mwa wapinzani, aligeuka na kutoa pasi kwa nyuma!

Goli walilolifunga Simba, Stima alikuwa katika nafasi nzuri ya kuuokoa mpira huo kabla ya kumfikia mfungaji, yeye alipeleka mguu kutaka kuupiga mpira huo lakini akaurudisha kabla ya kuupiga mpira huo ambao ulimfikia mfungaji na kufunga kirahisi sana!

Ni hali ya kawaida mchezaji kutokuwa katika ubora wake wa siku zote na kuigharimu timu kwa matokeo mabaya ambayo hayakutarajiwa! Lakini pia, ni kawaida uongozi wa Klabu kuzungumzia mapungufu waliyoyaona kusababisha matokeo mabaya kutokea! Inasikitisha, timu inapoelezea mapungufu waliyoyaona kama sababu ya kufanya vibaya kwa timu yao anaibuka mtu tu kutoka kusikojulikana akilalama, oooooh sijui maneno hayafai kusema public, kumsema mchezaji wako ni kumdhalilisha, sijui uletwe ushahidi.....Khaaaaaaa, jamani, yote haya yametoka wapi! Au lipo lililopo linalofanyika na anaeyasema haya na sasa anatafuta namna ya kujihami?

Yanga, enzi za rafiki yangu, mpendwa wangu sana Jerry Muro, ambaye namuombea TFF wamsamehe, arudi kazini, adhabu aliyoitumikia kwa mtazamo wangu imetosha kumpa funzo na kubadilika kwa yale aliyokengeuka, aliwahi kwa niaba ya uongozi wa timu yake kutangaza kumkataa mwamuzi asichezeshe mechi zao kwakuwa ilionekana hakuwa fair kwa upande wao.

Simba, kwa wenye kumbukumbu nzuri, waling'oa viti hao vya uwanja wa Taifa kwa kutoridhishwa na maamuzi ya waamuzi, hao hao Simba, walitaka baadhi ya mechi zao wachezeshwe na waamuzi kutoka nje ya nchi kwa maana kwamba, waamuzi ndani ya nchi kwa mechi hizo hawako fair!

Leo Ruvu Shooting kuzungumzia mapungufu katika maamuzi ya mwamuzi kwa mchezo dhidi yao imekuwa nongwa kwasababu, wao ni kuku, kunya kwao ni starehe na Ruvu Shooting ni bata, kunya kwao ni uchuro, siyo? Hii si sawa!

Sisi Ruvu Shooting tulidhani, yeyote anapolalamikia jambo lolote katika soka, kabla ya kumuita mlalamishi baada ya matokeo mabaya tuchunguze anachokilalamikia, tubaini ukweli ni upi kisha tuchukue hatua.

Ruvu Shooting hatuna kawaida ya kulalamikia waamuzi ila, inapotulazimu inatubidi tufanye hivyo ili kurekebisha mambo, waamuzi wachache wasiofuata maadili waondolewa, wanaharibu mpira wa Tanzania.

Ruvu Shooting tulifungwa goli 4-1 na Mbao FC nyumbani, Mabatini lakini tulimpongeza sana, tunaendelea kumpongeza tena sana Mwanahamisi Matiko kwa namna alivyochezesha mchezo ule kwa haki, ikizitafsiri Sheria 17 kikamilifu. Tungekuwa walalamishi kwa waamuzi, kwa nini husilalamikie Mwanahamisi aliyechezesha mechi tuliyofungwa goli nyingi kuliko mechi zote tulizocheza na badala yake tumpongeze? Acheni hizo, tushirikiane kuweka mpira wetu sawa. Pale mapungufu yanapojitokeza tukemee kwa pamoja.

Maneno kuhusu Mahagi kuwa na kadi ya uanachama Simba, yamesemwa sana na wengi, Mimi yalinifikia kupitia kwa watu mbalimbali wengine wa karibu sana na yeye! Nililifikisha kwa baadhi ya uongozi wa waamuzi, tukashauliana kishikaji kwa sababu nililipeleka kishikaji.

Katika Kanuni, sioni kama kuna katazo la kuzuia mtu yeyote mwenye uanachama na Klabu yoyote kuchezesha mpira, tumemdhuhudia enzi zake Inspector Hashimu ambaye alikuwa mwanachama wa Yanga alikini alikuwa mwamuzi na aliifanya vema kazi yake.

Tulichokisema Ruvu Shooting kuhusu mwamuzi mwenye uanachama na timu fulani ni mwamuzi huyo kutopangwa kuichezesha timu ambayo yeye ni mwanachama kwakuwa tayari ana maslahi binafsi katika timu hiyo.

Jingine ambalo lilizungumzwa ni kuhusu idadi ya mechi za Simba alizochezesha Mahagi. Hili watakaohitaji kwa faida yao wanaweza kufuatilia kupitia ratiba iliyotolewa. Ambalo kwetu sisi Ruvu Shooting halitupi shida kwani si la kikanuni. Hakuna mahala kanuni inasema mwamuzi katika mkondo mmoja wa ligi, kwa timu moja achezeshe mechi kadhaa! Hata akichezesha zote huyo huyo mmoja, haina shida, kanuni haimkatazi.

Rungu la Masau Bwire
Bwire alisikika kabla ya mchezo akiinadi timu yake kwamba, wanakwenda kumuangamiza Simba kwa kutumia Rungu, kauli ambayo iliwafanya watu wengi kuufuatilia mchezo huo kwa karibu ili kushuhudia namna ambavyo Rungu hilo litamuangimiza Simba! Dakika 90 zilipomalizika Shooting haikupata matokeo mazuri hivyo wakataka kujua, kulikoni Rungu limeshindwa kumumaliza Simba?

Majibu na sababu ya Rungu kushindwa kumumaliza Simba ziko wazi kabisa, walio kabidhiwa rungu walikosea kulishika wakati wa matumizi, badala ya kushika sehemu nyembamba (mpini) ili wambonde Simba kwa kichwa cha Rungu hilo, wao walishika kichwa cha Rungu na kujaribu kumshambulia Simba kwa ile sehemu nyembamba ya Rungu! Walirudi kulekule kwenye fimbo ya mwanzi!

Lakini vipi, ile kadi aliyopewa kipa wa Ruvu Shooting, haistaili kufutwa kama ilivyokuwa kwa yule wa pale mahala!

Imeandaliwa na;
Masau Bwire,
Afisa Habari wa Ruvu Shooting.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.