}

JESHI LA MAGEREZA TANZANIA BARA LAIPA MBINU ZA KUJITEGEMEA, CHUO CHA MAFUNZO ZANZIBAR.

 Na. Geofrey Jacka - Dodoma.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Meja Jenerali Suleiman Mzee, akimuelezea Jambo Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar, Luteni Kanali Khamis Bakari Khamis, (mwenye suti ya kijivu) alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato Dodoma.


Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar, Luteni Kanali Khamis Bakari Khamis, leo Julai 14, 2021 amefanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, kwa lengo la kujifunza namna ya uendeshaji wa Magereza na jinsi Jeshi hilo lilivyoweza kujitegemea na kuiondolea Serikali mzigo wa Madeni.

Katika kikao kilichoongozwa na Mwenyeji wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee, na baadhi ya Maafisa waandazi wa Jeshi hilo, Mzee alimsomea Luteni Kanali Khamis taarifa ya utendaji ya mwaka mmoja wa kujitegemea, ambayo inaonesha jitihadi mbalimbali na mafanikio yaliyo patikana tangu Jeshi lilipoanza kujiendesha lenyewe.


Baadhi ya Mambo yaliyoelezwa ni pamoja na  Mageuzi ya Kilimo ndani ya Jeshi, ambapo mitambo mbalimbali ya kuvunia mazao imenunuliwa kwa lengo la kurahisisha Uvunaji, Ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari zaidi ya 300 Tanzania nzima, Viwanda mbalimbali ikiwemo, Samani, Kuoka Mikate, Kiwanda cha kuchakata Mazao, huku taarifa hiyo ikionesha namna Askari na Wafungwa walivyoweza kutengeneza Gari iliyopata ajali na kuharibika vibaya, ambapo zaidi ya Magari 10  yametengenezwa na kuanza kufanya kazi.

Mara baada ya kikao hicho Meja Jenerali Mzee alimtembeza Luteni Kanali Khamis Bakari, katika maeneo mbali mbali ambayo miradi ya Ujenzi inaendelea, kama Kiwanda Cha Samani Msalato, Kiwanda Cha kuoka Mikate, Nyumba za makazi ya Maafisa na Askari, Ukumbi mkubwa na wa kisasa wa Sherehe na Mikutano, Kambi ya Kikosi maalumu cha Jeshi hilo,  Tanki kubwa la maji la ujazo wa zaidi ya Lita laki moja, pamoja na eneo la kibiashara na kucheza watoto lililopo Isanga.

Aidha Mzee amemueleza Luteni Kanali Khamis kuwa, Siri ya mafanikia yote ni kuanza kubadilisha fikra za Maafisa na Askari ili ziwe chanya, huku akisisitiza kutokaa Ofisini pekee, bali usimamizi thabiti, kutembelea miradi na kukagua mara kwa mara, ili kuona maendeleo yake.

 "My friend, ukikaa tu ofisini kwenye kiti Cha kuzunguuka, hakuna kitu kitafanyika, lazima utoke ukakague maendeleo ya miradi yako, hawa watu wetu wakati fulani bila ya kuwasimamia kisawasawa Mambo hayaendi" alisema CGP Mzee.

Akizungumza mara baada ya kutembelea miradi yote, Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Zanzibar Luteni Kanali Khamis Bakari Khamis amesema, amejifunza mengi katika ziara hii, huku akichukua nafasi hiyo pia kumshukuru Kamishna Jenerali wa Magereza Meja Jenerali Suleiman Mzee kwa uthubutu wake wa kuanzisha miradi mikubwa kwa fedha za ndani, huku akiahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Jeshi hilo na Vyuo vya Mafunzo Zanzibar.

"Nimejifunza vitu vingi Sana kwenye hii Ziara, ni siku moja lakini niliyojifunza ni kama nimekaa chuo mwaka mzima, nilikuwa namwambia msaaidizi wangu hapa, hawa wanaofanya haya sio Malaika, ni binadamu kama sisi, hivyo lazima nasisi tukafanye kazi Sasa, tena natamani nibebe maafisa wangu wote wa Mafunzo pia waje waone Mambo yanayofanyika hapa, na nikuahidi tuu sitajifungia ofisini, nafikiri Sasa hata Mafaili nitakuwa naletewa Saiti" alisema Kamishna Khamis.
Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Luteni Kanali Khamis Bakari, akiangalia mitambo katika Kiwanda Cha Samani Msalato.

Ziara ya Luteni Kanali Khamis itaendelea hapo kesho Alhamisi Julai 14, kwa kutembelea Gereza kuu Isanga Dodoma, na kuzungumza na Wafungwa na Mahabusu, pamoja na Miradi ya Ujenzi inayoendelea kutekelezwa na Gereza hilo.

Tazama Picha Zaidi.


No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.