}

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU(NBS) YATANGAZA KUPUNGUA KWA MFUMUKO WA BEI NCHINI.

Na.Happy Shirima-Dar.
Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Machi, 2018 umepungua hadi kufika asilimia 3.9 ikilinganishwa na asilimia 4.1 ya mwezi februari hi ikiwa ni kwa mujibu wa ofisi ya taifa ya Takwimu (NBS).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini dar es salaam Mkurugenzi wa sensa ya watu na Takwimu za jamii Ephraim Kwesigabo amesema kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioisha mwezi Machi imepungua ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa mwaka ulioisha mwezi februari 2018.

Bw. Kwesigabo amesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi ambapo mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula  umechangia kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioisha mwezi Machi.

Aidha baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kati ya Machi,2017 na Machi  2018 ni pamoja na mtama asilimia 7.1, maharage asilimia 3.9, mihogo mibichi asilimia 16.6 na ndizi za kupika asilimia 16.7.

Kwa upande wa mfumuko wa bei  kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki umeonyesha kupungua ambapo Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioisha mwezi machi 2018 umepungua hadi asilimia 2.0 kutoka 2.1, huku Kenya ukiwa 4.18 kutoka asilimia 4.46 kwa mwaka ulioisha mwezi februari 2018.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.