}

WANANCHI WAMETAKIWA KUTOA TAARIFA JUU YA MABANGO YENYE KUAMBATANA NA TAARIFA ZA UONGO

Wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona mabango ya matangazo barabarani ambayo wanayatilia shaka.

Haya yanasemwa jijini Dar-es-salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na watu wenye Ulemavu Mh. Janista Mhagama alipokuwa akizungumzia uwepo kwa utitiri wa mabango ya ajira yanayoambatana na ahadi za uongo kwenye mishahara.

Alisema kuwa sheria za uwekaji mabango barabarani zinazoongozwa na mamlaka husika zikiwemo Serikali za Mitaa, Halmashauri ya Jiji na Miji ambazo huweka kanuni na taratibu za mabango hayo.

“Mamlaka husika zina wajibu wa kujiridhisha na kuhakikisha mabango yanayopewa ruhusa kubandika barabarani ni sahihi, yanatangaza ukweli na yanafuata maadili” alisema Mhe. Mhagama.

Waziri Mhagama aliongeza kuwa ikibainika kuwa mabango hayo yanakwenda kinyume na utaratibu waliokubaliana, mamlaka husika wana wajibu wa kuyafuatilia na kuyaondoa mabango hayo ili kuondoa usumbufu usiowa lazima kwa wananchi.

Akizungumzia suala la mabango yanayotangaza ajira yanayoambatana na ahadi za uongo, Mhe. Mhagama amesema kuwa kuwa wizara yake ndiyo yenye dhamana ya ajira, inabidi wawasiliane na mamlaka husika ambazo zimeruhusu mabango hayo ili wafuatilie na kuchukua hatua stahiki.

Aidha, alizungumzia ukaguzi unaofanywa na wizara yake mahali pa kazi alisema kuwa wao hawafuatilii mabango bali huenda kufuatilia kama mwajiri anafuata sheria za kazi ikiwemo mikataba, mishahara, afya na kupeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi za jamii.

“Tunapokuta malalamiko ya wafanyakazi, au kukuta mwajiri hapeleki michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya jamii, kuna adhabu za hapo kwa hapo kama vile kumtoza mwajiri pesa” alisema Mhe. Mhagama.

Katika kuhakikisha utendaji kazi unaridhisha na maridhiano sehemu za kazi Mhe. Mhagama alisema kuwa wao kama wasimamizi wakuu wa ajira nchini wanafanya kazi kwa karibu na shirikisho la vyama vya wafanyakazi na waajiri, ili kutatua kero za wafanyakazi katika sehemu zao za kazi.


Kwa upande wake Mstahiki Meya wa jiji la Dar-es-Salaam Mhe. Isaya Mwita alisema kuwa utaratibu wa kuweka mabango upo kisheria katika halmashauri ila usumbufu mkubwa ni kuwa matangazo madogo madogo ambayo mengi yanawekwa kwenye karatasi za A4 ambayo yanabandikwa kwenye kuta za nyumba, nguzo za umeme na miti bila kufuata utaratibu.


“Kwa sasa tunafanya utaratibu wa kukutana na viongozi wa jiji wakiwemo madiwani, wenyekiti wa halmashauri, wenyekiti wa wilaya na wengine ili kuweka utaratibu wa kudhibiti matangazo hayo, pamoja na kuweka sheria ndogo ndogo, na hivyo kuwapunguzia kero wananchi ambao wanaumizwa na matangazo hayo” alisema Mhe. Mwitta.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.