}

POLISI,MAHAKAMA,NA WAPELELEZI WAPEWA ELIMU JUU YA BIASHARA HARAMU YA BINADAMU

KATIBU wa Sekretarieti ya Kitaifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Separatus Fella, amewataka Maafisa Wapelelezi wa Jeshi la Polisi, Mahakimu na Waendesha Mashtaka nchini watumie mbinu za kisasa za Kupeleleza, Kuendesha na Kusikiliza kesi dhidi ya Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu.
Akuzungumza katika Hoteli ya land Mark, iliyopo Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya siku tano kwa wanasheria hao yaliyoandaliwa na Taasisi ya Wanasheria Wasio na Mipaka (Lawyers Without Borders) ya nchini Marekani, Fella alisema, Tanzania ni kati ya mataifa yanayoshamiri kwa biashara hiyo hivyo mafunzo yaliyotolewa na Taasisi hiyo yataleta mwanga zaidi kwa wanasheria hao nchini.
“Nawaomba washiriki wote wa mafunzo haya, kuzingatia na kutumia kwa usahihi utaalamu mlioupata katika kupambana na tatizo hili la biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu ambalo linaendelea kukua kwa kiwango kikubwa,” alisema Fella.
Fella aliongeza kuwa, Tanzania ni kati ya mataifa yanayoshamiri kwa biashara haramu ya ikiwemo ya usafirishaji watoto ikiwa na lengo la kwenda kuwatumikisha kazi katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na duniani kwa ujumla, kutokana na changamoto hiyo, Serikali ina mipango mbalimbali ya kupambana na tatizo hilo ambalo linazidi kukua kila siku.
Hata hivyo, Fella alisema licha ya changamoto mbalimbali ya kupambana na biashara hiyo, lakini ofisi yake imejipanga kikamilifu kupambana na biashara hiyo kwani maafisa wake wana ujuzi na wanaendelea kupata ujuzi wa kupambana na biashara hiyo na pia wanaendelea kutumia nyenzo mbalimbali za utoaji elimu kwa umma juu ya matatizo hayo nchini.
Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu nchini Marekani, Virginia Kendall ambaye ni mmoja kati ya wataalamu waliotoa mafunzo kwa maafisa hao, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa kipaumbele cha upambanaji wa biashara hiyo haramu na pia elimu waliyoitoa wataalamu hao kwa wanasheria hapa nchini itasaidia kuongeza kasi kubwa ya kupambana na biashara hiyo. 
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliratibu mafunzo hayo kwa lengo la kujipanga kikamilifu katika kupambana na biashara hiyo haramu ambayo inazidi kuleta mateso makubwa kwa idadi kubwa ya Watanzania. 
Pia Mwezi Oktoba mwaka jana, Wizara hiyo iliandaa Warsha ambayo ilifadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) ambayo ililenga kujadili nyenzo mbalimbali ambazo zitasaidia kuwalinda na kuwasaidia watoto walioathirika na biashara ya kusafirisha binadamu  nchini.
Nyenzo hizo zililenga kuwasaidia na kuwalinda watoto walioathirika baada ya kutoka katika maeneo mbalimbali zinatarajiwa kusaidia kutoa elimu zaidi ya kuwandaa kisaikolojia watoto hao ili wasikate tamaa na maisha, pia watoto watalindwa na baadaye watarudishwa kwa wazazi wao kutoka sehemu mbalimbali ndani ya nchi na nje ili waweze kuendelea na majukumu mengine ya kujenga taifa.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.