JUMUIYA YA WAZAZI YAKAMILISHA UCHAGUZI.
WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM),wamemchagua tena Najma Murtaza Giga kuwa Mbunge wa Viti Maalum Zanzibar kwa kura 591 na kuwaacha mbali wapinzani wake watano.
Aidha,kwa upande wa Bara,Wajumbe hao wamemchagua Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS),Dokta Catherine Joachim kwa kura 567 kati ya kura halali 708 zilizopigwa.
Akitangaza matokeo hayo Agosti Mosi,2025,Jijini Dodoma Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara,John Mongela amesema kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, wajumbe waliwachagua Aza Joseph na Salama Abasi Juma kushika nafasi za uwakilishi kwa Viti Maalum.
"Ndani ya chama chetu wote ni washindi haijalishi umepata kura ngapi hivyo asitokee mtu kujisifia kuwa yeye ni mshindi lakini pia kura hizi hazimaanishi kuwa tayari mmekuwa wabunge kwani mchakato wa chama utakamilika baada ya vikao vya juu vitakapo keti na kutoa maamuzi ya mwisho,"amesema Mongela.
Katika uchaguzi huo Hadija Taya maarufu kama Keisha, ambaye pia alikuwa Mbunge wa Viti Maalum, hakufanikiwa kurejea bungeni.
Uchaguzi huo ni sehemu ya mchakato wa ndani ya chama wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
No comments