JESHI LA ZIMAMOTO LATOA ELIMU MAGEREZA.
Na. Geofrey Jacka - Morogoro
Jeshi la Zima Moto na uokoaji mkoani Morogoro kupitia kitengo cha Habari na Elimu kwa Umma, leo Oktoba 12, 2021, kimetoa Elimu na Mafunzo juu ya namna ya kupambana na Majanga hasa ya Moto, kwa Askari Wanafunzi wa kozi namba moja ya Sajini awamu ya tatu, yanayofanyika katika Chuo cha Magereza KPF mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa utoaji elimu hiyo Mtaalamu kutoka Jeshi la Zimamoto Sajini Benjamini ameeleza kuwa, Jeshi hilo limekuwa na majukumu mengi, ikiwa ni pamoja na kukagua Ramani za majengo na kutoa ushauri wa namna ya ujenzi utakao zingatia usalama pindi majanga yanapotokea, huku msingi wake mkubwa ukiwa ni kuokoa maisha ya Raia na mali zao hasa wakati wa majanga
Sajini Benjamini akielezea Jambo Mara baada ya kufika chuo KPF kwaajili ya kutoa elimu ya kukabiliana na Majanga hasa ya Moto.
Aidha Benjamini ametoa ushauri kuwa jamii ziwe na utamaduni wa kuwa na vifaa vya kukabiliana na Majanga ya Moto, huku akisisitiza nyumba ziwe na milango ya kuingilia na kutokea zaidi ya mmoja ili kurahisisha utokaji pindi majanga yanapotokea, huku akisema kuwa kwa majengo yanayotumika na watu wengi Kama Mabweni ni lazima milango yake iwe inafunguka kwa kusukuma kwenda nje pindi watu wanapotaka kutoka.
"Siwezi kuongelea Sana milango ya Magereza yetu, lakini kuhusu Mabweni ya shule na Majengo mengine yanayotumiwa na watu wengi lazima milango ifunguke kwa nje, na pia tusiruhusu majani kusogelea karibu na nyumba, lazima tuweke mipaka ili hata ukitokea moto basi ufike sehemu uzimike, na hata kwenye mashamba makubwa, tunashauri kuweka barabara ili kupunguza athari pindi Moto unapotokea" aliongeza Sajini Benjamini.
Katika utoaji wa elimu hiyo, askari wanafunzi wa kozi namba moja ya Sajini wa Magereza inayoendeshwa chuo cha Magereza KPF, walipata nafasi ya kuuliza Maswali na kupatiwa ufafanuzi na Mtaalamu huyo, ambapo waliaahidi kwenda kuitumia elimu hiyo katika shughuli za kila siku pindi watakaporejea katika vituo vyao Mara baada ya kuhitimu Mafunzo.
No comments