}

WAZIRI MKUU AZIAGIZA HALMASHAURI,MANISPAA NA MAJIJI KUTENGA MAENEO YA MAZOEZI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (aliyevaa traksuti nyeupe) akiwa ameongozana na Viongozi mbalimbali kuelekea Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kwenye Uzinduzi wa Kitaifa wa Mazoezi ya Viungo kwa Wananchi wote yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma leo 11/02/2017.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (wa pili kulia), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu (wa pili kushoto) pamoja na Viongozi wengine wakifanya mazoezi kuelekea Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kwenye Uzinduzi wa Kitaifa wa Mazoezi ya Viungo kwa Wananchi wote yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma leo 11/02/2017.



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa a
meziagiza Halmashauri, Manispaa na Majiji yote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya wananchi kufanya mazoezi na kupumzika.

Kassim Majaliwa ametoa agizo hilo leo, Mjini Dodoma wakati wa Uzinduzi wa Kitaifa wa Mazoezi ya Viungo kwa Wananchi wote yaliyofanyika katika viwanja vya Jamhuri.

"Ni muhimu kufanya mazoezi kila siku, mazoezi yanasaidia kuchangamsha mwili, kufahamiana, kujenga urafiki pamoja na kuwa na afya bora," alisema Mhe. Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema kwamba, muitikio wa ufanyaji mazoezi wa viungo ni mkubwa, ambapo watu wengi wamejiunga na vikundi mbalimbali vya kufanya mazoezi ya viungo.

Aidha, amezitaka Halmashauri, Manispaa na Majiji yote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya watu kufanya mazoezi na kumpuzika.
Ameongeza kuwa, watu wasilazimishwe kufanya mazoezi bali iwe ni hiari ya yao na kusiwe na gharama kwa ajili ya mtu kufanya mazoezi.

Vile vile amewataka Maafisa Utamaduni na Michezo nchini kuhamasisha mazoezi ya viungo katika maeneo yao pamoja na kuanzisha vikundi vya mazoezi ya viungo ambapo watakuwa wanakutana na kufanya mazoezi kwa muda ambao watajipangia.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amemshukuru Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha mazoezi ya viungo na kuitangaza rasmi Jumamosi ya pili ya kila mwezi kuwa ni siku ya mazoezi ya viungo Kitaifa.
Aliendelea kwa kusema kuwa, mazoezi ya viungo yanamuepusha mtu na kupata magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo, kisukari pamoja na saratani.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amesema kwamba, mazoezi ya viungo yanaratibiwa na Wizara ya Habari, Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI. Hivyo kwa pamoja watahamasisha uanzishwaji wa vikundi vya mazoezi ya viungo katika Halmashauri zote nchini kwa kuanza na watumishi wa Umma.

Aidha amewataka viongozi wanapokuwa mikoani katika siku ya mazoezi ya viungo wawahamasishe wananchi kufanya mazoezi ya viungo kwa ajili ya kulinda afya zao.

Uzinduzi wa Kitaifa wa mazoezi ya viungo ulianza kwa matembezi yaliongozwa na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuanzia viwanja vya Bunge na baadaye alimkabidhi Waziri Mkuu kuanzia Nyerere Square mpaka Uwanja wa Jamhuri. Uzinduzi huo umehusisha viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Viongozi wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Wananchi wa Mkoa huo.
Share: 






















No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.