TANZANIA KUWA NA MASHIRIKA YA UMMA YENYE USHINDANI IFIKAPO 2050
Ifikapo mwaka 2050, Tanzania inajiona kuwa na Mashirika ya umma ya kibiashara yanayoendeshwa kwa uwazi na ushindani, yanayojitegemea na yenye kuleta faida, na yanayovutia uwekezaji huku yakishirikiana kikamilifu na sekta binafsi ili kukuza uchumi.
Dhamira hii imeainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa na Rais. Dk. Samia Suluhu Hassan, jijini Dodoma katika tukio lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Nehemiah Mchechu, ambaye ni Msajili wa Hazina.
Ofisi ya Msajili wa Hazina ndio imepewa jukumu la kuhakikisha ndoto hiyo ya kuyajengea mashirika ya umma ya kibiashara nguvu ya kuwa shindani inafikiwa, kwakuwa ndio msimamizi wa uwekezaji wa mashirika hayo.
Inasimamia jumla ya Taasisi, Mashirika ya umma na wakala wa serikali 252, ambapo kati ya hizo, 217 zinatoa huduma na 35 zinafanya biashara.
“Mashirika haya yamekuwa yakipata ruzuku kutoka Serikalini, jambo linaloondoa mazingira ya ushindani kati yao na kampuni binafsi. Hali hii imesababisha kupungua kwa ufanisi wa sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya taifa,” inasema sehemu ya Dira ya Taifa 2050.
Dira 2050 inaenda mbali kwa kuonesha haja ya kuwa na mfumo wa uwekezaji unaobainisha maeneo ya uwekezaji kati ya mashirika ya umma ya kibiashara na sekta binafsi ili kuharakisha ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.
No comments