TANZANIA INA UMEME WA KUTOSHA–DKT.BITEKO
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dokta Doto Biteko, amesema Tanzania ina umeme wa kutosha baada ya kukamilika kwa Miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ukiwemo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere, ambao pekee unazalisha Megawati 2115.
Naibu Waziri Mkuu amesema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua ya miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II Jijini Dar es Salaam.
Amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na TANESCO baadhi ya maeneo yalikabiliwa changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini mpaka sasa yameendelea kuimarika.
Dokta Biteko amefafanua kuwa upatikanaji wa umeme unaendana na mahitaji ya ongezeko la watu na TANESCO inatarajia kuongeza uzalishaji umeme katika Kituo cha Kinyerezi III kutoka megawati 600 katika mpango wa awali hadi kufika Megawati 1000.
Aidha, Naibu Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza TANESCO kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ya kuwahudumia wateja hasa kwa uharaka wao wa kukabiliana na dharula zozote za umeme zinazojitokeza.
Vilevile, Dkt. Biteko ametembelea Kituo cha Kupokea Gesi Asilia Kinyerezi kwa ajili ya kukagua miundombinu ya kusafirisha gesi na kuwataka kuongeza uzalishaji wa gesi ili kusaidia kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Biteko aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo katibu Mkuu wa Wizara ya nishati, Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange.
No comments