PWANI KUGAWA VYANDARUA ZAIDI YA 970,000, WANANCHI MIL. 1.6 KUNUFAIKA
MKOA wa Pwani unatarajia kugawa vyandarua 971,939 katika kampeni ya ugawaji wa vyandarua bure kwa kaya 426,637, kampeni itakayoanza Agosti 15, 2025.
Kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini ifikapo mwaka 2030.
Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Menejimenti , Serikali za Mitaa, Utawala na Fedha, George Nsajigwa, amesema hayo wakati akizindua kampeni ya uhamasishaji na ugawaji vyandarua mkoani Pwani kwa niaba ya Katibu Tawala mkoani humo katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Nsajigwa ameeleza kuwa kampeni hiyo itatekelezwa katika kata 108 na vijiji/mitaa 426, ambapo kaya 426,637 zenye jumla ya watu takribani milioni 1,633,774 watanufaika.
“Kampeni hii inalenga kutokomeza malaria nchini, na inaratibiwa kwa pamoja na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bohari ya Dawa (MSD), pamoja na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI,” ameongeza Nsajigwa.
Peter Gitanya, kutoka Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), ameeleza, Serikali imeweka mkakati madhubuti kuhakikisha kila kaya inapokea vyandarua bora vya kujikinga na mbu waenezao malaria.
Akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe – Dkt. Rashid Mfaume, Stella Kanyange kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, amesema nchi , imepunguza ugonjwa wa maralia kwa asilimia 15 mwaka 2017 ambapo kwa mwaka 2022 imeshuka kwa asilimia 45 na kufikia asilimia 8.1.
Mwisho
No comments