KILIO CHA MUDA MREFU CHA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI CHAMFIKIA RAIS DKT SAMIA -MAVUNDE
Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, amesikia kilio cha muda mrefu cha wachimbaji wadogo wa madini kuhusu kupatiwa maeneo ya uchimbaji yaliyoko ndani ya leseni ya serikali.
Katika hilo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, amezielekeza mamlaka kutoa leseni ya uchimbaji madini ya Nikeli kwa Shirika la Madini la Taifa-STAMICO, pamoja na wachimbaji wadogo wa eneo la Vilima vya Ntaka, Nachingwea, Mkoani Lindi.
Waziri Mavunde, ametoa taarifa hiyo katika mkutano uliofanyika Kijiji cha Nditi, baada ya kutembelea maeneo na migodi ya wachimbaji wadogo wanaojumuika chini ya Umoja wa Vikundi vya Wachimbaji Madini-UVIWAMA.
Aidha, amewataka wachimbaji wadogo kufuata taratibu kama zinavyoelekezwa katika Sheria ya Madini Sura ya 123, ikiwemo kuhakikisha wanapata ridhaa ya wenye haki za kimila za ardhi kabla ya kuanza uchimbaji, ili kuepusha migogoro.
Rais Dokta Samia, ameelekeza eneo la leseni lenye ukubwa wa kilometa za mraba 45 likabidhiwe kwa STAMICO kwa ajili ya kuanza uchimbaji mkubwa wa madini ya Nikeli ndani ya miezi 18, kama sheria inavyotaka.
No comments