}

JESHI LA POLISI NA CALTEX WASHIRIKIANA KUPUNGUZA AJALI BARABARANI

Waendesha Pikipiki na Bajaji nchini wametakiwa kujifunza kwa kina Sheria za Usalama Barabarani pamoja na kupata maarifa sahihi ya matumizi ya barabara kabla ya kuingia barabarani kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Usalama Barabarani Chang’ombe, Reverent Nkyami, wakati wa uzinduzi wa kilainishi kipya cha Caltex Ezy 4T Plus kilichozinduliwa rasmi wilayani Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Nkyami amesema ukosefu wa elimu rasmi na mafunzo ya usalama barabarani umechangia waendeshaji wengi wa pikipiki kuendesha vyombo hivyo kiholela bila kuzingatia sheria, hali inayochochea ongezeko la ajali na vifo barabarani.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi limeendelea na juhudi za kutoa elimu kwa waendesha vyombo vya moto pamoja na kufanya oparesheni mbalimbali, zenye lengo la kuongeza uelewa kwa madereva na kupunguza ajali barabarani.


Aidha, amewataka waendesha pikipiki kushiriki kikamilifu kwenye mafunzo yanayoendeshwa na Jeshi hilo ili kuongeza maarifa, weledi na kuwa salama wawapo barabarani.

Kwa upande mwingine, uzinduzi wa kilainishi kipya cha Caltex Ezy 4T Plus uliambatana na uzinduzi wa kampeni ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda na bajaji. Kilainishi hicho kimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na kimekusudiwa kupunguza gharama za matengenezo ya vyombo vya moto.

Mkuu wa Kitengo cha Vilainishi kutoka Kampuni ya Karimjee Value Chain Limited, Anam Mwemutsi, amesema bidhaa hiyo mpya imekuja kupambana na tatizo sugu la uchakachuaji wa vilainishi linalosababisha uharibifu wa injini za pikipiki.

Naye Msemaji Msaidizi wa Shirikisho la Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Msisiri, amepongeza kampuni hiyo kwa kubuni suluhisho litakalosaidia kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri na kupunguza ajali zitokanazo na ubovu wa pikipiki.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.