CANADA YAIPA TANZANIA DOZI MIL 23 ZA VITAMINI A.
Serikali ya Canada kupitia Shirika lake linaloshughulika na masuala ya lishe duniani la Nutrition International imetoa dozi milioni 23 za vitamini A yenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 kwa Serikali ya Tanzania ili kuokoa maisha kwa kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya maradhi kwa watoto.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mjumbe wa Bodi wa Shirika la Nutrition International, ambaye pia ni Rais mstaafu wa Awamu ya Tano, dokta Jakaya Kikwete kwenye Kituo Cha Afya Cha Makuburi akiwa na ujumbe wa Canada ulioongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa Randeep Sarai.
Katika Hotuba yake Mhe. Dkt. Kikwete ameipongeza Serikali ya Canada kwa kuendelea kuwa mshirika wa kweli katika kuisaidia Tanzania katika eneo la Afya.
Aidha, amefafanua kwamba Serikali ya Canada imeendelea kuwa mfadhiri mkuu katika eneo hili kutokana na ukweli kuwa Serikali ya Tanzania ni Serikali makini inayoaminika na mataifa mbalimbali duniani.
Kwa upande wake, Sarai amesema mataifa haya mawili ya Canada na Tanzania yamekuwa na mahusiano mazuri katika Sekta ya Afya ambapo amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania.
Awali Naibu Waziri wa TAMISEMI anayeshughulikia eneo la Afya, Festo Dugange ameishukuru Serikali ya Canada kwa mchango mkubwa kwenye eneo la afya hususan usajili wa watoto chini ya miaka mitano hapa nchini.
Amesema, vituo vya kuandikishia watoto vimeongezeka kutoka 139 mwaka 2013 hadi 12,025 Julai 2025 hivyo kupunguza umbali wa kutoka kituo kimoja hadi kingine kuwa ndani ya kilomita 5–6 kutoka kilimita 80–140 mwaka 2013.
No comments