HOSPITALI YA TEMEKE YAANZA MAFUNZO YA UPASUAJI KWA NJIA YA TUNDU NDOGO
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke imeanza rasmi kutoa mafunzo kwa wataalamu wake wa afya hasa madaktari bingwa wa upasuaji, mifupa, magonjwa ya ndani na mabingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kuhusu mbinu ya kisasa ya upasuaji kwa kutumia tundu ndogo maarufu kama Laparoscopy.
Mafunzo haya yaliyoanza mapema wiki hii yana lengo la kuwajengea uwezo madaktari hasa wa upasuaji na wauguzi wanaohudumu katika idara ya upasuaji ili kuimarisha utoaji wa huduma za upasuaji kwa njia salama, ya haraka na yenye maumivu madogo kwa mgonjwa.
Akizungumzia kuhusu kuanza kwa mafunzo hayo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke Dkt. Joseph Kimaro amesema kuwa mbinu hiyo ni sehemu ya mkakati wa hospitali kuboresha huduma za kibingwa kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mgonjwa ambapo Hospitali kwa kuwezeshwa na serikali imetumia kiasi cha fedha milioni mia tano ishirini na tano fedha za makusanyo kununua mashine hiyo ya Laparoscopy ambayo imenunuliwa kupitia MSD.
"Kupitia mafunzo haya, tunalenga kupunguza muda wa kulazwa kwa wagonjwa na kuongeza ufanisi katika huduma za upasuaji. Hii ni hatua muhimu kuelekea maboresho ya huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke na Mkoa wa Dar es Salaam," amesema Dkt. Kimaro.
Dkt. Hussein Msuma, Daktari Bingwa wa Upasuaji na Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke, amesema mafunzo haya yamefungua ukurasa mpya katika utoaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi
“Kupitia mafunzo haya ya Laparoscopy, tunatarajia kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa wetu kwa kupunguza muda wa kupona, hatari ya maambukizi na gharama za kulazwa. Ni hatua kubwa ya kimaendeleo kwa hospitali yetu na kwa mfumo mzima wa afya nchini. Tunaamini baada ya kuanza rasmi kwa huduma hii, tutapunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali ya taifa ya Muhimbili na kuwahudumia wananchi wetu kwa ufanisi zaidi hapa Temeke.” Alisema Dkt. Msuma
Laparoscopy ni njia ya upasuaji inayofanyika kwa kufanya matundu madogo tumboni na kutumia vifaa maalum kuangalia na kutibu matatizo mbalimbali bila kufungua tumbo lote, Mafunzo haya yamejumuisha wataalamu wa afya kutoka vitengo mbalimbali vya upasuaji, na yanatarajiwa kuchukua muda wa wiki moja hadi kukamilika na hatimaye huduma hii kuanza rasmi kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke.
No comments