DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050 YAZINULIWA TANZANIA NA RAIS DKT. SAMIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania haikuweza kutimiza malengo ya dira mbalimbali ilizoweka awali kutokana na sababu kadhaa zikiwemo mapungufu ya usimamizi wa sheria, utegemezi wa fedha za nje na athari za sera za kiuchumi wa dunia.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo wakati akizungumza katika uzinduzi wa Dira ya Taifa 2050 jijini Dodoma.
Amebainisha kuwa majanga ya kiuchumi ya kidunia yamechangia kurudisha nyuma juhudi za maendeleo.
Hata hivyo, ameeleza kuwa serikali sasa imejipanga kwa kuhakikisha dira mpya inatekelezwa kikamilifu.
Aidha, ameeleza kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa kujenga uwezo wa kiuchumi na kifedha wa taifa, sambamba na kuweka mikakati imara ya kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi inayoweza kujitokeza duniani.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Watanzania wote kujielekeza katika kutekeleza kwa vitendo Dira ya Taifa 2050 badala ya kuishia kwenye maneno.
Rais Dkt. Samia amesema tabia hiyo haimhusu mtu mmoja au kundi fulani, bali ni changamoto ya kitaifa inayohitaji kushughulikiwa kwa pamoja.
"𝙏𝙪𝙣𝙖𝙥𝙤𝙯𝙞𝙣𝙙𝙪𝙖 𝘿𝙞𝙧𝙖 2050, 𝙩𝙪𝙟𝙞𝙚𝙡𝙚𝙠𝙚𝙯𝙚 𝙠𝙖𝙩𝙞𝙠𝙖 𝙫𝙞𝙩𝙚𝙣𝙙𝙤 𝙯𝙖𝙞𝙙𝙞 𝙠𝙪𝙡𝙞𝙠𝙤 𝙢𝙖𝙣𝙚𝙣𝙤, 𝙬𝙖𝙯𝙚𝙚 𝙬𝙚𝙩𝙪 𝙬𝙖𝙡𝙞𝙨𝙚𝙢𝙖 𝙡𝙞𝙨𝙤𝙡𝙤𝙗𝙪𝙙𝙞 𝙠𝙪𝙩𝙚𝙣𝙙𝙬𝙖 𝙣𝙖 𝙝𝙖𝙬𝙖𝙠𝙪𝙨𝙚𝙢𝙖 𝙡𝙞𝙨𝙞𝙡𝙤𝙗𝙪𝙙𝙞 𝙠𝙪𝙨𝙚𝙢𝙬𝙖, 𝙨𝙖𝙨𝙖 𝙩𝙪𝙣𝙖 𝙩𝙖𝙗𝙞𝙖 𝙮𝙖 𝙠𝙪𝙨𝙚𝙢𝙖 𝙨𝙖𝙣𝙖 𝙠𝙪𝙡𝙞𝙠𝙤 𝙠𝙪𝙩𝙚𝙣𝙙𝙖.."
Aidha, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa ili dira mpya iwe na mafanikio, ni lazima serikali, sekta binafsi, na wananchi kwa ujumla washirikiane kwa vitendo, kila mmoja akitimiza wajibu wake.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dokta Hussein Ally Mwinyi amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha dira ya 2050 inazinduliwa.
Amesema kuzinduliwa kwa dira hiyo ni muelekeo wa miaka 25 ijayo, inayofanya ndoto, matarajio na matamanio ya watanzania yanatimia.
Rais Mwinyi, ameyasema hayo wakati anatoa salamu zake kwenye uzinduzi wa dira ya Taifa 2050 yenye kauli mbiu ustawi wa pamoja.
Na Makamu wa Rais Dokta Philip Mpango amesema maendeleo ya Taifa lolote haiitaji kuwa ya majaliwa wala kuachia nguvu ya soko bali hujangwa kwa fikra bunifu.
Aidha Dokta Mpango amesema nchi zote zinazofanikiwa kwa maendeleo inatokana na kuwepo kwa Dira ya muda mrefu sambamba na kufuatilia utekelezaji wa yale mliojiwekea katika Dira ya Taifa ya Maendeleo .
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dokta Kitila Mkumbo amesema Shabaha kubwa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni Kuwa Tanzania kuwa na pato lenye thamani ya dola za marekani Trillion-1 na wastani wa pato la mtu mmoja lenye thamani ya dola Marekani Elfu- 7 baada ya wataalam wa ndani na nje ya nchi kukaa na kuangalia kutokana na hali ya uchumi wa nchi kuwa kufikia mwaka 2050 mtanzania anaweza kufikia kipato hicho kwa mwaka.
Aidha shabaha nyingine ni kuhakikisha Umaskini uliopitiliza kwa watanzania, Watanzania kuishi wastani wa miaka 75 wakiwa wenye afya pamoja na pamoja na kupata huduma bora za afya kwa wote.
No comments