WIZARA YA KILIMO IZIWESHE TAASISI KUPATA ZANA ZA KISASA - WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo iweke utaratibu wa kuziwezesha taasisi zinazojihusisha na kilimo kwa kuzipatia zana za kisasa za kilimo ili kukuza sekta hiyo.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza tija katika shughuli za kilimo zinazofanywa na taaaisi hizo. “Mitambo hii ya kupandia, kuvunia pamoja na umwagiliaji ina gharama kubwa sana, lakini Wizara yetu ya Kilimo ikiweka utaratibu mzuri wa kuziwezesha hata kwa mkopo itazisaidia kuzalisha kwa tija.”
Ametoa agizo Jumapili, Agosti 03, 2025, wakati akizungumza na wadau wa ushirika na wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Kitaifa yaliyofanyika katika Kijiji cha Ushirika, kwenye viwanja vya maonesho ya NaneNane, Nzughuni, jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wakulima kwa mwaka 2025.
Amesema taasisi kama Magereza, JKT ambazo zinafanya shughuli za kilimo zikipatiwa zana hizo kwa mikopo, zitawawezeshwa kuwa na teknolojia za kisasa jambo ambalo wasingeweza kulifanya kwa kutumia fedha zao.
Akizungumzia kuhusu ushirika, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, yaani misimu ya kilimo ya 2023/2024 na 2024/2025, nchi imeshuhudia mafanikio makubwa yanayodhihirisha nguvu ya ushirika katika kuleta tija kwenye sekta ya kilimo na kuinua maisha ya wananchi. Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za pamoja kati ya Serikali, vyama vya ushirika, na wanachama.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema utendaji wa ushirika nchini uko salama na umebadilika sana hadi kufikia hatua ya baadhi ya vyama kuweza kununua mazao, kubangua na kuuza nje ya nchi.
Amesema kutokana na ufanisi unaoendelea kuonekana kwenye tasnia ya ushirika, Wizara hiyo hivi sasa inalenga kuongeza thamani na kwamba baada ya miaka mitatu ijayo, inatarajia kuona baadhi ya SACCOS zinageuka kuwa benki.
Katika hatua nyingine, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege amemshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kusimamia urejeshaji wa mali za ushirika hali ambayo imechangia kuimarishwa kwa ushirika nchini.
No comments