}

WANANCHI ZAIDI YA 29,000 WAFIKIWA KATIKA KAMBI ZA MATIBABU BILA MALIPO PEMBA

 


Mke wa Rais, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi, ameeleza kufarijika na mwitikio mkubwa wa kuwafikia wananchi zaidi ya 29,000 ambapo shabaha iliyowekwa awali ilikuwa wananchi 25,000 katika kuwapatia huduma za kibingwa na huduma za msingi za afya bila malipo.



Mama Mariam Mwinyi amesema hayo leo tarehe 15 Agosti 2025 alipofunga Kambi ya Tano ya Matibabu ya Afya Bora, Maisha Bora, iliyofanyika katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Vitongoji, Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba.


Aidha, amepongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, katika kuimarisha huduma za afya nchini, ikiwemo ujenzi wa hospitali katika kila wilaya na kukamilisha ujenzi wa hospitali kubwa kwa kila mkoa.


Amesema kambi za matibabu na matembezi ni miongoni mwa shughuli zinazotolewa na Taasisi ya ZMBF. Ameeleza kuwa programu nyingine zinazotekelezwa na ZMBF ni pamoja na uwezeshaji wa wanawake na vijana wakulima wa mwani, kupinga ukatili wa kijinsia, pamoja na programu za afya na lishe.


Vilevile, ametoa wito kwa wananchi kufuatilia ratiba za kambi za matibabu zinazotolewa katika kila wilaya na mkoa ili waendelee kupata huduma kupitia kambi hizo.


Kwa upande mwingine, amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani nchini, hususan kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.



















No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.