MICHEZO YA KUBAHATISHA SI CHANZO CHA AJIRA NI BURUDANI TU
Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) imesisitiza kuwa michezo ya kubahatisha siyo mbadala wa ajira bali ni burudani tu, na hivyo wananchi wanapaswa kucheza kwa kiasi ili kuepuka uraibu unaoweza kusababisha madhara ya kijamii na kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma wa GBT, Daniel ole Sumayan, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Sumayan amesema, licha ya sekta ya michezo ya kubahatisha kuwa changa hapa nchini, bado inaendelea kukua kutokana na kuongezeka kwa uelewa na uhitaji wa burudani hiyo miongoni mwa jamii.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri amesema mikutano kama hiyo ni jukwaa muhimu la kuimarisha mawasiliano kati ya taasisi za umma na vyombo vya habari, ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu shughuli za serikali.
Kikao hicho kililenga kuonesha mafanikio ya GBT chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
No comments