MADALALI WA MINADA WATAKIWA KUJISAJINI KIELEKTRONIKI.
Wizara ya Fedha imeandaa Mfumo wa Kielektroniki wa utoaji Leseni za Udalali na Uendeshaji minada ya hadhara unaowezesha uombaji na upatikanaji wa Leseni kwa njia ya kielektroniki kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta mpakato ili kuwaondolea wananchi adha na gharama ya kufuata leseni hizo jijini Dodoma.
Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Jijini Dodoma, Msimamizi wa Mali za Serikali wizarani hapo, Bw. George Killo, alisema Mfumo huo utamuwezesha mwananchi kufanya usajili popote alipo hivyo kupata leseni yake kwa wakati.
‘‘Mwombaji wa leseni ya udalali anapaswa kujisajili kupitia Tovuti ya Wizara ya Fedha (www.mof.go.tz) na kisha kubonyeza kipengele cha GAMIS na kujisajili, kujaza taarifa zinazohitajika, kujaza fomu za maombi kikamilifu na kuwasilisha kwa Katibu Tawala wa Wilaya husika kwa ajili ya uhakiki na Saini,’’ alieleza Bw. Killo.
Alisema mwombaji wa Leseni za Udalali na Uendeshaji Minada ya hadhara anahitajika kuwa na fomu ya maombi iliyojazwa kikamilifu na kugongwa muhuri na Katibu Tawala wa Wilaya husika, Tax Clearance Certificate/incorporation, leseni ya biashara pamoja na Tax Clearance Certificate na viambatisho hivyo viwe katika mfumo wa PDF.
Alisema kupitia mfumo huo mwombaji anaweza kupata taarifa za maombi yake ikiwa yametumwa, yamekataliwa au yamekamilika na waombaji waliofanikiwa wataorodheshwa katika Tovuti ya Wizara ya Fedha na kuchukua leseni zao katika Ofisi ya Usimamizi wa Mali za Serikali katika mikoa yao.
‘‘Leseni hizi zinazotolewa na Wizara ya Fedha zinatumika katika uendeshaji wa minada ya hadhara, ukusanyaji wa madeni, ushuru, tozo, udalali wa mahakama, udalali wa nyumba na viwanja ambapo hutolewa kwa muda wa mwaka mmoja (Januari -Disemba) kwa Sh. 150,000/= na nusu mwaka (Januari – June) (Julai – Disemba) kwa Sh.75,000,’’ alifafanua Bw. Killo.
Alisema dalali yoyote ambaye anaendesha mnada wa hadhara kwa upande wa Tanzania Bara anatakiwa awe amesajiliwa na awe na leseni halali ambayo haijaisha muda wake wa matumizi inayotolewa na Wizara ya Fedha.
Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi zilizo chini yake inashiriki katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo na Uvuvi 2025’’.
No comments