}

KAYA 3,255 KUNUFAIKA NA MAJIKO YA GESI YA RUZUKU WILAYA YA MLELE

Wananchi Kijiji cha Usevya Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini-REA katika kuhakikisha wanafikiwa na nishati safi ya kupikia kwa bei ya ruzuku.

Wametoa pongezi hizo wakati wa usambazaji wa majiko ya gesi-LPG ya kilo sita na vichomeo vyake kwa bei ya ruzuku ya shilingi 19,500 kwa kila jiko.

Kwa upande wake, Christina Sindano, mkazi wa Kijiji cha Usevya amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa mstari wa mbele katika kampeni hiyo ambayo alisema inanufaisha wananchi wake hususan kina mama.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Usevya, Focus Kapongwa, amesema wananchi kijijini hapo wamekuwa na mazoea ya kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa lakini kufika kwa mradi kutapunguza ukataji holela wa miti.

Akizungumza kuhusu mradi, Mtaalam wa Jinsia na Nishati wa Wakala wa Nishati Vijijini-REA, Dkt.Joseph Sambali, amesema mradi huo kwa Mkoa wa Katavi unatekelezwa kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa Gas Limited ambapo jumla ya majiko 9,765 ya gesi-LPG yatasambazwa.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Mlele, Yahaya Mbulu, ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ikiwemo ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao na kuhifadhi mazingira.

"Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele kwenye Niishati Safi ya Kupikia; inakadiriwa kuwa takribani watu 31,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati isiyo salama," alibainisha Mbulu.

REA inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wameachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.