}

WIZARA YA AFYA YAJADILI RASIMU YA MPANGO MKAKATI WA KUBORESHA ELIMU YA AFYA KWA UMMA

Wizara ya Afya kupitia Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma imeandaa kikao kazi maalum kwa ajili ya kupitia na kuidhinisha rasimu ya mpango mkakati wa kuboresha elimu ya afya kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya ya jamii kupitia uelewa wa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo Julai 14, 2025 jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkuu wa kikao kazi hicho, Dkt. Norman Jonas, amesema mchakato wa uandaaji wa rasimu hiyo ulianza rasmi mwaka 2024.

 Amefafanua kuwa hatua ya sasa inalenga kukusanya maoni ya wadau na kamati kabla ya kuanza kwa utekelezaji rasmi.

Dkt. Jonas amesema kuwa rasimu hiyo, inayotarajiwa kuanza kutumika kuanzia Septemba mwaka huu, inalenga kuweka misingi madhubuti ya utoaji wa elimu ya afya kwa umma kwa njia bora na za kisasa ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mbinu za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza pamoja na yale yasiyoambukiza.

 “Tunachofanya sasa ni hatua muhimu za mapitio na maboresho mengine kabla ya kuanza utekelezaji wa mpango huu. Tunalenga kupata maoni ya wadau mbalimbali ili kuhakikisha mkakati wetu wa utoaji wa elimu ya afya kwa umma unakuwa wa kisasa, wenye kueleweka na wenye msaada mkubwa katika kuzuia magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza,”  amesema Dkt. Jonas.

Aidha, amesema kuwa rasimu hiyo imeangazia umuhimu wa kutumia majukwaa ya kidijitali na mitandao ya kijamii kama njia mbadala ya kufikisha elimu ya afya, hasa kwa vijana na makundi maalum katika jamii.

 Imeelezwa kuwa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) yataleta mapinduzi katika upashanaji wa taarifa, sambamba na kuimarisha uwezo wa Serikali kufuatilia uelewa na mabadiliko ya tabia katika jamii.

Wakichangia katika majadiliano, baadhi ya washiriki wamesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa viongozi wa kijamii, na vyombo vya habari katika utekelezaji wa mkakati huo

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.