WANAFUNZI MCHEPUO WA KIINGEREZA WADAIWA ADA ZAIDI YA MIL. 168
Shule ya Msingi Mkoani yenye mchepuo wa Kiingereza, Kata ya Tumbi katika Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani, inakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha kutokana na wazazi kushindwa kulipa ada kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Adelhelma Shawa, amesema shule hiyo inadai jumla ya Sh. Milioni 168.9 kutoka kwa wazazi wa wanafunzi.
Shawa ameeleza, kati ya kiasi hicho, sh.milioni 51,563,000 ni madeni ya miaka ya nyuma ambayo baadhi ya wazazi wamekuwa wakiyapunguza taratibu.
Nae Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amefafanua, shule hiyo inatakiwa kujiendesha kwa mfumo wa shule binafsi, na kwa sasa kuna mpango wa kuwaondoa walimu wote wa Serikali na kuajiri walimu wa moja kwa moja kupitia shule hiyo.
Mmoja wa wazazi, Omari Salehe, ambaye mtoto wake anasoma katika shule hiyo, amesema uwepo wa shule hiyo ni msaada mkubwa kwao kwa kuwa mtoto anapata elimu bora kwa gharama ndogo ikilinganishwa na shule nyingine binafsi.
Shule hiyo ya serikali ilianzishwa mwaka 2018 kwa lengo la kutoa elimu bora kwa mchepuo wa Kiingereza kwa gharama nafuu, ikilinganishwa na shule nyingine binafsi, ili kuwapa watoto wa Kitanzania fursa sawa ya kielimu.
Mwisho
No comments