}

RAIS SAMIA ATOA BILIONI NNE UJENZI KIWANDA CHA KUZALISHA NISHATI MBADALA

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) leo tarehe 22 Julai, 2025 wamesaini mkataba wenye lengo la kujenga kiwanda kipya cha kuzalisha nishati mbadala (Mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes) mkoani Geita ambapo mkataba huo una thamani ya shilingi bilioni 4.5.

Katika hafla iliyofanyika katika Ofisi ndogo ya REA, Jijini, Dar es Salaam, REA itatoa jumla ya shilingi bilioni tatu na STAMICO itatoa shilingi bilioni 1.5; kwa mchanganuo huo, REA itagharamia ununuzi wa mtambo wakati STAMICO italipia upatikanaji wa kiwanja, ujenzi wa jengo la kiwanda na gharama za ufungaji wa mitambo. 

Mkataba huo umesainiwa na Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse.


Mkataba huo utaifanya STAMICO kuwa na viwanda vikubwa vitano vya kuzalisha mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes; viwanda vingine ambavyo vinaendelea na uzalishaji wa mkaa mbadala vipo wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani, Kiwira mkoani Songwe, na viwanda vingine viwili vipo mkoani Dodoma na Tabora ambapo vipo kwenye hatua za mwisho za ukamilishwaji kabla kuanza uzalishaji. 

Akizungumza  katika hafla hiyo, Mhandisi, Hassan Saidy, amesema kuwa Wakala umepewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia unafikia asilimia 80 kwa Watanzania wote ifikapo mwaka 2034. 


Mhandisi, Saidy ameongeza kuwa Wakala unaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ili kuhakikisha Mkakati wa Nishati safi ya kupikia unatimiza malengo yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji na usambazaji wa mkaa mbadala, Wakala unaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo usambazi wa majiko banifu, usambazaji wa majiko ya umeme, usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia majumbani (LPG ya kilo 6 na 15); usambazaji wa gesi asilia katika mkoa wa Lindi na Pwani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi za Umma. 

Kwa upande wake, Dkt. Venance Mwasse, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO ameishukuru Serikali kupitia REA kwa mchango huu ambao utasaidia Shirika hilo  kutimiza ndoto yake ya kuhakikisha wananchi wote wanaachana na nishati isiyo safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034 na hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali za kutunza mazingira.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.