RAIS SAMIA ATOA BILIONI 16 KWA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA ELIMU TANGA
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025, imetoa shilingi Bilioni-16.696 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari-SEQUIP, Mkoani Tanga.
Kati ya fedha hizo, shilingi Bilioni-4.450 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Tanga, ambayo tayari imekamilika.
Miundombinu hiyo ni madarasa 22, maabara, mabweni 12, bwalo la chakula, jengo la utawala na nyumba tano za walimu.
Kaimu Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Tanga, Mwalimu Joel Laizer, amesema serikali imetoa pia shilingi Bilioni-1.6 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Mkoa ya Amali katika Wilaya ya Mkinga, ambapo ujenzi unaendelea kwa kasi.
Kiasi cha shilingi Bilioni-3.505 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule sita za Amali katika halmashauri tano, ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Tanga, Mwalimu Chuki Athumani, pamoja na Mwalimu wa TEHAMA, Obed Mndota, wameipongeza serikali kwa kazi kubwa ya kujenga shule hiyo kwa kiwango na ubora wa hali ya juu, ikiwa na miundombinu yote muhimu ya kitaaluma na kijamii.
Wanafunzi Anjela Cosmas, na Jessica Mussa, nao wametoa pongezi kwa Serikali huku wakisema ndoto zao zinaonekana kutimia kutokana na maboresho makubwa ya miundombinu shuleni.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Parungukasera kilichopo Wilaya ya Mkinga, Neema Mashimba, amesema ujenzi wa shule ya Amali unaendelea kwa kasi na kukamilika kwake kutasaidia kuongeza ufanisi wa elimu na ujuzi kwa watoto wengi wa eneo hilo.
No comments