}

MIKOA, WILAYA ZATAKIWA KUSIMAMIA KIKAMILIFU MIRADI YA UBORESHAJI VITUO VYA AFYA

Serikali imeagiza viongozi wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanasimamia kwa karibu miradi ya ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya unaoendelea nchini, ili utekelezwe kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati.

Rai hiyo imetolewa Julai 22, 2025 na Afisa kutoka Idara ya Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Bi. Faraja Mgeni, wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya mradi wa ukarabati wa vituo vya Afya vya Mbande na Mzinga (wilaya ya Temeke), pamoja na Kituo cha Afya Kimbiji na Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Bi. Faraja amesema jukumu la kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo si la waganga wafawidhi peke yao, bali ni la viongozi wote wa mikoa na wilaya kwa ujumla.

"Ni lazima viongozi wa mikoa na wilaya wahakikishe wanashiriki kikamilifu katika kusimamia kila hatua ya ukarabati wa vituo hivi. Tunahitaji usimamizi wa karibu ili miradi hii iwe na matokeo chanya kwa wananchi,” amesema Bi. Faraja

Amesema kuwa kuwa ukarabati huo unaotekelezwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Suzan Thompson Buffett Foundation (STBF), unalenga kuboresha huduma za afya ya uzazi kwa akina mama na watoto wachanga.

Maeneo yanayofanyiwa ukarabati ni pamoja na vyumba vya kuhudumia akinamama waliopoteza ujauzito, vyumba vya watoto wachanga mahututi na njiti na wodi za kujifungulia.

Pia, Bi. Faraja ameongeza kuwa, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, ameelekeza kila kituo cha afya kuwa na eneo la kufulia la kisasa kwa ajili ya akina mama waliomaliza kujifungua.

“Hili ni agizo la moja kwa moja kutoka kwa Waziri wa Afya. Eneo la kufulia linahitajika ili kuimarisha huduma na mazingira baada ya kujifungua kwa kina mama wetu,” amesema.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali imejipanga kuongeza vifaa tiba vipya katika vituo hivyo mara baada ya ukarabati kukamilika, kwa lengo la kuboresha zaidi huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.

Mradi wa ukarabati wa vituo hivyo unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 30, 2025, na ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na kusogeza huduma bora karibu na wananchi.

No comments

Haki zimehifadhiwa. Copyright, kituochahabari.com ©2016. Blog designed by Geofrey Donatus Jacka.. Powered by Blogger.