KONGAMANO LA MABARAZA YA HABARI LAINGIA SIKU YA TATU, AI YATAJWA MWELEKEO USIOEPUKIKA
Kongamano la Mabaraza ya Habari Barani Afrika limeingia siku ya tatu leo jijini Arusha, Tanzania, ambapo mjadala umejikita katika matumizi sahihi ya Akili Unde(AI), huku wadau wa habari kutoka mataifa zaidi ya 30 wakisisitiza kuwa teknolojia hiyo sasa haiepukiki.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema licha ya juhudi zilizopo katika kutoa mafunzo kuhusu matumizi ya AI kwa waandishi wa habari, bado kuna haja ya kuongeza nguvu zaidi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia.
“Ni wazi kuwa AI si jambo la kupuuzia. Hatuwezi kuizuia, bali tunapaswa kuhakikisha waandishi wa habari wanajengewa uwezo wa kuielewa na kuitumia kwa weledi,” alisema Balile.
Katika siku ya pili ya kongamano hilo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, alilifungua rasmi na kusisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya Akili Unde. Alieleza kuwa mabadiliko ya teknolojia hayaepukiki, hivyo kuna umuhimu wa kutoka na maazimio ya namna bora ya kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari barani Afrika.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, ameishukuru Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo muhimu, akieleza kuwa limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kushirikisha mataifa takriban 30 kutoka bara la Afrika.
“Ushiriki mpana wa mataifa mbalimbali unaonesha hamasa ya pamoja ya kukuza tasnia ya habari Afrika kupitia mijadala ya kitaaluma na ya kimkakati kama huu,” alisema Sungura.
Kongamano hilo linatarajiwa kuhitimishwa kesho , ambapo washiriki kutoka mataifa mbalimbali watapata fursa ya kutembelea vivutio kadhaa vya utalii.
No comments